1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki na Ujerumani zakubaliana juu ya Wakimbizi wa Syria

8 Februari 2016

Nchi hizo mbili zimekubaliana kuchukua hatua ya kuzuia wimbi la wakimbizi wa kutoka Syria, zikijumuisha juhudi za pamoja za kidiplomasia za kuzuia mauaji yanayoendelea kushuhudiwa katika mji wa Aleppo.

https://p.dw.com/p/1HrZx
Kansela Merkel na waziri mkuu Davutoglu mjini Ankara
Kansela Merkel na waziri mkuu Davutoglu mjini AnkaraPicha: Reuters/U. Bektas

Ujerumani na Uturuki zimelaani mashambulio ya angani yanayofanywa na Urusi pamoja na vikosi vya rais Bashar al Assad katika mji wa Aleppo nchini SyriaWaziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu amesema nchi yake na Ujerumani zimekubaliana kuchukua hatua ya kuzuia wimbi la wakimbizi wa kutoka Syria,hatua ambazo zitajumuisha juhudi za pamoja za kidiplomasia za kuzuia mauaji yanayoendelea kushuhudiwa katika mji wa Aleppo.

Kansela Angela Merkel ambaye kwa pamoja na mwenyeji wake waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu wamekutana na waandishi wa habari mjini Ankara leo(Jumatatu) mchana amesema wameshtushwa na hali ya mateso yanayowakabili watu nchini Syria kutokana na mashambulizi ya angani yanayofanywa na Urusi. Ametanabahisha kwamba matumizi ya nguvu yanayoshuhudiwa nchini Syria yanabidi kukomeshwa haraka iwezekanavyo akitaja kwamba vitendo vya Urusi vinakwenda kinyume kabisa na azimio la Umoja wa Mataifa ambalo limetilia mkazo wa kuzuiwa mashambulizi dhidi ya raia.

Ajali ya boti la wakimbizi wa Syria katika eneo la bahari la mpaka Kati ya Uturuki na Ugiriki
Ajali ya boti la wakimbizi wa Syria katika eneo la bahari la mpaka Kati ya Uturuki na UgirikiPicha: Getty Images/AFP

''Katika kipindi cha siku chache zilizopita sio tu tumeshangazwa lakini pia tumeshtushwa na kile ambacho kimesababisha mateso ya maelfu ya watu kutokana na mabomu na hasa yanayofanywa na upande wa UrusiKwa hali kama hiyo mazungumzo ya kutafuta amani ni vigumu kufanyika.Na hii ndio sababu inabidi kuikomesha mara moja''

Waziri mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu kwa upande mwingine amezungumzia juu ya Ujerumani na Uturuki kukubaliana kuhusu hatua za kuzuia wimbi la wakimbizi kutoka Syria.Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Uturuki nchi hizo mbili zitaanzisha juhudi za pamoja za kuitia msukumo Jumuiya ya kujihami ya Nato kuhusika zaidi katika suala la wakimbizi,ikimaanisha kwamba Nato itahitajika kutumia uwezo wake kuwa mwaangalizi katika mipaka ya Syria na eneo la Bahari ya Meditterinea.

Pamoja na Hilo waziri mkuu huyo wa Uturuki amesema nchi yake haiwezi kutarajiwa kuubeba peke yake mzigo wa wakimbizi wakati wasyria kiasi 30,000 wamepiga kambi katika mpaka wa Uturuki baada ya kukimbia mashambulizi ya angani ya nayofanywa na Urusi pamoja na wanajeshi wa serikali ya Assad kaskazini mwa mkoa wa Aleppo.Kansela Merkel amemuunga mkono waziri mkuu Davutoglu akisema ni sahihi kabisa kwamba haiwezi kufikiriwa kwamba Uturuki peke yake kwasababu inawapokea wakimbizi basi inabidi ilibebe jukumu hilo na kulishuhughulikia suala hilo peke yake.

.Umoja wa Ulaya umekuwa ukiishinikiza Uturuki kufungua milango yake kuwapokea mamia kwa maelfu ya wakimbizi wakisyria waliomiminika katika mpaka wake wakikimbia vita na mauaji yanayoendelea Aleppo. Mpaka sasa Uturuki imeshawapokea wakimbizi milioni 2.5 wa Syria na inasema haina uwezo tena wakuwashughulikia wakimbizi zaidi ingawa imeonesha kuwa tayari kuwapokea wakimbizi zaidi.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman