1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uturuki: mzozo wa Qatar unahujumu ulimwengu wa Kiislamu

Caro Robi
14 Juni 2017

Msemaji wa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema mzozo unaoizonga Qatar unahujumu ulimwengu wa Kiislamu na Uturuki inafanya jitihada za kusaidia kuutatua mzozo huo kwa njia ya kidiplomasia

https://p.dw.com/p/2ei4W
Emir Tamim von Qatar und Erdogan
Picha: Picture alliance/dpa/Turkish President Press Office

Akizungumza katika mkutano na wanahabari Ibrahim Kalin, msemaji wa Rais Erdogan amesema nchi yake inatuma msaada wa chakula Qatar baada ya nchi za ghuba kusitisha uhusiano nayo na kuiwekea vikwazo kwa madai kuwa inaunga mkono ugaidi na inashirikiana na Iran ambayo ni hasimu wa nchi za ghuba, madai ambayo Qatar imeyakanusha.

Kalin pia amefafanua kuwa kambi ya kijeshi ya Uturuki iliyoko Qatar ambayo ilianzishwa hata kabla ya mzozo huo kati ya Qatar na majirani zake ilianzishwa kwa lengo la kuhakikisha usalama katika kanda hiyo na sio kutumika kijeshi dhidi ya nchi yoyote.

Rais Erdogan leo amemtuma waziri wake wa mambo ya nje Mevlut Cavusoglu Qatar katika juhudi za kuutanzua mzozo huo alioulaani akisema unakwenda kinyume na misingi ya Kiislamu.

Malta EU-Außenministertreffen | Mevlut Cavusoglu, Türkei
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki yuko QatarPicha: picture-alliance/Anadolu Agency/C. Ozdel

Cavusoglu atakutana na mfalme wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad al Thani katika ziara hiyo ambayo pia itamfikisha Saudi Arabia. Uturuki inaunga mkono Qatar katika mzozo huo ambao umezihusisha nchi kadhaa na kusababisha athari mashariki ya kati, Misri hadi Iraq na kuibua wasiwasi Marekani na Urusi.

Kamishna mkuu wa tume ya kutetea haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad al Hussein amesema anatiwa wasiwasi mkubwa na athari zitakazojitokeza kutokana na kutengwa kwa Qatar na majirani zake Saudi Arabia umoja wa falme za Kiarabu, Bahrani pamoja na Misri akionya huenda ikasababisha mateso kwa raia wa kawaida, akiongeza ni bayana hatua zilizochukuliwa ni kali mno na zimevuka mipaka.

Wakati huo huo, Qatar imesema imeyaondoa majeshi yake katika mpaka kati ya nchi za Djibouti na Eritrea ambako taifa hilo la kiarabu lilikuwa mpatanishi katika mzozo wa mipaka kati ya nchi hizo mbili za Afrika. Djibouti ilitangaza imepunguza uhusiano na Qatar.

Kusitishwa huko kwa uhusiano na vikwazo dhidi ya Qatar, taifa lenye idadi ya watu milioni 2.7 na tajiri la gesi, limetatiza kuingizwa kwa chakula na bidhaa nyingine nchini humo na kusababisha baadhi ya benki za kigeni kupunguza biashara zake nchini humo.

Qatar ambayo huagiza asilimia 80 ya chakula chake kutokwa kwa majirani zake waliositisha uhusiano imeziomba Iran na Uturuki kuipa chakula na maji.

Mwandishi: Caro Robi/reuters/afp
Mhariri:Yusuf Saumu