Utunzaji mazingira: Waokotaji taka Dakar
Nchini Senegal, maelfu ya waokotaji taka huwa wanapekuwa moja ya jaa kubwa kabisa wakitafuta plastiki na taka nyingine wanazoweza kuuza. Lakini eneo hilo lina hatari kubwa kimazingira.
Msako wa taka za plastiki na chuma
Watu wapatao 2,000 wana kawaida ya kuokota taka katika jaa la Mbeubeuss ambalo liko nje kidogo ya mji mkuu wa Senegal, Dakar. Wanasaka taka za plastiki zinazoweza kutumiwa tena, au huwa wanachoma baadhi ya taka nyingine wakitafuta mabaki ya vyuma vyenye thamani.
Wauzaji wa jumla wananunua taka zinazoweza kutumika tena
Waokotaji taka hawa wanapata faida kwa kuwauzia wafanyabiashara ya jumla taka zinazoweza kutumika tena. Baadhi yao wanaweza hata kupata faranga 100,000 kwa mwezi (sawa na €150/$180). Kipato hicho ni cha nchini Senegal, lakini wengi wanapata faida ndogo zaidi ya hiyo.
Harufu mbaya ya taka mbichi
Ili kujipatia riziki, waokotaji taka hawa wanakabiliana na joto kali lakini pia harufu mbaya ya taka. Kila siku, wanasubiri malori yatupe taka kwenye jaa hilo. Kisha wanaanza kuokota haraka iwezekanavyo.
Ng'ombe wakitafuta chakula kwenye jaa la taka
Kwa jumla, malori 230 huleta karibu tani 1,300 za taka kwenye jaa hilo kila siku. Taka hizo pia huvutia ng'ombe na ndege, ambao hutangatanga kwenye eneo hilo la hekta 114 (ekari 280) kutafuta chakula.
Waokotaji taka siku zote wanadhulumiwa
Pape Ndiaye, msemaji wa chama cha waokota taka, anasema hali inazidi kuwa ngumu kujipatia riziki kwenye jaa hilo la Mbeubeuss. Licha ya ushindani ulioko, kuna shida ya kuanguka kwa bei ya jumla ya taka hizo. Ingawa wanaoziokota wanasaidia kuyalinda mazingira lakini "wao ndiyo siku zote wanaodhulumiwa", ameliambia shirika la habari la Agence France-Presse.
Hatari ya kimazingira
Jaa la taka la Mbeubeuss linajulikana kuwa linahatarisha mazingira. Waokotaji wanapochoma moto taka, moshi wenye sumu husambaa kwenye eneo lote, na kufikia maeneo ya makazi. Ziwa lilioko nje kidogo ya jaa hilo limegeuka rangi nyekundu kutokana na uchafuzi wa mazingira.
Jaa la Mbeubeuss linakaribia kufungwa
Lakini baada ya kulipuuza jaa hilo la Mbeubeuss kwa miongo kadhaa, serikali ya Senegal sasa imeamua kulifunga eneo hilo. Mnamo mwaka 2025, litageuzwa kuwa kituo cha kutenganisha taka. Kwa waokotaji taka hilo litakuwa ni pigo kubwa.