Utawala wa kijeshi wa Guinea, watangaza serikali mpya.
15 Januari 2009Utawala huo wa kijeshi umetangaza serikali hiyo, ikiwa ni wiki ya tatu sasa, tangu kufanyika kwa mapindizi hayo ya kijeshi, Desemba 23.
Kapteni Moussa Dadis Camara, ambaye alishika madaraka mwezi uliopita, ameiitangaza serikali hiyo mpya yenye mawaziri wapatao 30, kutoka pande zote za Jeshi na raia.
Lakini hata hivyo katika uteuzi huo, hakuna wawakilishi wowote kutoka vyama vya siasa waliojumuishwa katika serikali hiyo.
Kati ya Mawaziri hao 29, 10 ni wanajeshi, akiwemo Kapten Mamadou Sande, ambaye anakuwa Waziri wa Uchumi na Fedha, wizara ambayo itakuwa chini ya Ofisi ya Rais.
Nafasi nyeti ya Wizara ya Madini, kutokana na umuhimu kwamba nchi hiyo inaongoza duniani, kwa kusafirisha nje madini ya Aluminium, inashikwa na Mahmoud Thiam, wakati wizara inayoshughulika na masuala ya ulinzi ikishikwa na Mamadouba toto Camara na masuala ya Jeshi yakishikwa na Sekouba Konate, ambayo yako chini ya Ofisi ya Rais.
Uteuzi wa Mawaziri hao katika serikali mpya, umetokana na matakwa ya kiongozi huyo wa kijeshi nchini humo, Moussa Dadis Camara, ambaye alishika nafasi hiyo, muda mchache baada ya kufariki kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Lasana Konte, baada ya kuongoza nchi hiyo toka mwaka 1984.
Desemba 30, mwaka ulioisha, utawala huo wa kijeshi nchini Guinea, ulimteua pia Kabine Komara, Mkurugenzi wa zamani wa benki, kushika nafasi ya Uwaziri Mkuu.
Maafisa vijana wa jeshi la nchi hiyo wakiongozwa na Kapten Camara wametoa ahadi ya kutokomeza rushwa nchini humo, uvunjaji wa haki za binadamu, pamoja na kuangalia upya mikataba ya madini nchini humo.
Awali Utawala huo wa kijeshi uliahidi kufanya uchaguzi mwaka 2010, licha ya Rais Abdoulaye Wade wa nchi jirani ya Senegal, ambaye pia aliwaunga mkono viongozi hao wa kijeshi kushauri uchaguzi kufanyika mapema.
Kufanyika kwa mapinduzi hayo ya Guinea, kulisababisha Jumuia ya Kimataifa hususan katika nchi za Afrika, kuulaani na kutoukubali utawala huo.
Umoja wa Afrika ulitamka kuwa uamuzi huo wa Kapteni Camara wa kutwa madaraka ni haramu, kutokana na kwamba unakiuka katiba ya nchi hiyo na kutangaza kuisimamisha nchi hiyo katika uanachama wa Umoja huo, hadi hapo utawala unaozingatia katiba utakaporudishwa nchini humo.
Katika hatua nyingine bado utawala huo wa kijeshi, unawashikilia watu 20, wakiwemo maafisa wa kijeshi 14, walio bado watiifu kwa serikali ya zamani , ya Rais Lansana Conte.
Wakati utawala huo, ukijidhatiti kwa kuunda serikali, miongoni mwa mada zitakazojadiliwa katika Mkutano ujao wa Umoja wa Afrika, utakaofanyika Adids Ababa Februari mosi hadi tatu, ni pamoja na kujadili mapinduzi ya kijeshi ya Guinea.
Guinea ilisimamishwa uanachama katika umoja huo mara tu baada ya mapinduzi hayo, ikiwa ni nchi ya pili kuchukuliwa hatua hiyo na umoja wa Afrika unaopinga utwaaji madaraka kwa matumizi ya nguvu.
Nchi nyengine ni Mauritania, ambako wanajeshi waliuangusha utawala uliochaguliwa kidemokrasi wa Rais Sidi Ould Cheikh Abdillahi Agosti mwaka jana.