Utafunaji mirungi Somaliland
Mmea wa mirungi umeambatanishwa sana na utamaduni wa watu wa Somaliland kiasi cha kwamba umekuwa sehemu ya maisha ya kiuchumi ya nchi hiyo. Wakosoaji wanalalamikia athari ya kileo hiki kwa familia.
Baada ya nishai
Kiasi cha asilimia 90 ya watu wazima wanaume wa Somaliland wanatafuna mirungi wakitafuta 'mirqaan' - neno la Kisomali linalomaanisha nishai - inayoweza kupatikana kwenye kileo hiki. "Marafiki zangu hunikopesha pesa," alisema Abdikhalid alipoulizwa anawezaje kupata mirungi ilhali hana kazi. "Nikipata kazi tu, nitarejesha fadhila."
Kichochea nguvu
"Nahofia athari za kiafya lakini inanisaidia kwenye kazi," anasema Nayfar ambaye kawaida hufanya kazi usiku. Mwandishi wa habari Abdul huitafuna anapokabiliwa na muda wa mwisho kuwasilisha kazi. "Ni bora kuliko pombe kwani baadaye unaweza kufanya kazi kawaida," anasema huku meno yakiwa kijani kwa kutafuna mirungi. "Inawaathiri watu kwa namna tafauti - wengine hupenda kusoma, wengine kufanya kazi."
Mama mirungi
Kawaida wateja hununua mirungi kwa wale waitwao 'mama mirungi', wanawake wanaoendesha biashara mitaani. "Nina duka na mkahawa na nilianza kuuza mirungi kwani nilitaka kutanua biashara yangu," anasema Zahre Aidid, mama mirungi kwa mwaka wa 22 sasa. Biashara ni nzuri. Ana kibanda chake cha mirungi kandoni mwa cha daktari wa meno, ambapo wateja hutumia kiasi cha dola 6 hadi 10 kwa siku kwa mirungi.
Mirungi na vita vya wenyewe kwa wenyewe
"Wanawake wengi waliiingia biashara ya mirungi baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kwani ilikuwa ndio njia pekee ya kuzikimu familia," anasema Aidid. "Baada ya kuanza kuifanya, wakajua namna ya kuifanya vyema zaidi, hivyo wakaendelea. Wanawake kadhaa sasa wanauza mirungi." Takribani asilimia 20 ya wanawake wa Somaliland pia wanatafuna mirungi na idadi inaongezeka. Kawaida wao hutafuna faraghani.
Mirungi 'Express'
Mirungi hupandwa kaskazini mashariki mwa Ethiopia na kutoka huko husafirishwa kwa magari yanayopita kwenye barabara mbovu katika jangwa la Somaliland. Vibanda vya mirungi kawaida huwa na namba za kupendeza ili kumtambulisha msambazaji na kuwapa wateja uchaguzi. "Kuna kiasi cha namba 5,000," anasema mteja mmoja kwenye kibanda cha mirungi cha wateja 725.
Athari za kiuchumi
Uchumi wa mirungi umepangwa vizuri sana Somaliland kiasi cha kwamba umekuwa sehemu muhimu ya kodi kwa serikali. "Mwaka 2014, bajeti ya Somaliland ilikuwa dola milioni 152 ambapo asilimia 20 ilitoka kwenye mirungi," anasema Weli Daud wa Wizara ya Fedha. Lakini hilo haliwazuwii wakosoaji kulalamikia athari za mirungi kwa kuzichafua familia na kuihusisha na tabia chafu na mapigano majumbani.
Familia zateseka
"Mwanamme anakuwa si sehemu ya familia na mwanamke anaachwa afanye kila kitu," anasema Fatima Saeed, mshauri wa kisiasa. "Wanaume wanatumia masaa kadhaa kutafuna mirungi - ni kilevi kabisa. Mirungi inaweza kusababisha wazimu, kukosa usingizi, kupoteza hamu ya kula na matatizo mengine." Anasema kuipiga marufuku mirungi moja kwa moja ni jambo lisilo na uhalisia lakini uwekwaji wa sheria utasaidia.
Kuitetea mirungi
"Mirungi inawaleta watu pamoja, inachochea mijadala juu ya masuala mbalimbali na kubadilishana taarifa," anasema Abdul. "Unakotoka ni tabu kwa watu kujikusanya pamoja lakini hapa wanajua kuhusu majirani zao na matatizo waliyonayo." Haiwezekani kuwa Ethiopia ingeliwataka Wasomaliland waache kukusanyika na kutafuta mirungi: mauzo ya mwaka ya mirungi kwa Somaliland ni dola milioni 524.
Utafunaji waendelea
"Siitukani mirungi kwani ni biashara yangu," anajibu Aidid juu ya mashaka ya mirungi. Saeed alisema serikali ya sasa haitaweka sheria zozote. Hivyo biashara inaendelea kwani kila siku wanaume hutoweka kwa masaa na kuishia kwa marafiki kutafuna mirungi. Kutafuna majani hayo kulichukuliwa kama jambo tukufu na Wamisri wa kale. "Kuifahamu hasa mirungi, unapaswa kuitafuna," anasema Nayfar.