1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utafiti wa maoni ya umma nchini Afghanistan

Oumilkher Hamidou12 Januari 2010

Asili mia 75 ya waafghanistan 1554 walioulizwa maoni yao wanahisi nchi yao inafuata njia inayofaa

https://p.dw.com/p/LRav
Bunge la AfghanistanPicha: DW

Kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka chungu nzima,wananchi wa Afghanistan wameanza kujiwekea matumaini mema. Licha ya matumizi ya nguvu yanayoendelea,wengi wa wananchi wa Afghanistan wanahisi nchi yao inafuata njia inayofaa. Hayo ni matokeo ya utafiti wa maoni uliofanywa kwa mara ya tano na vituo vya televisheni vya Ujerumani ARD na WDR kwa ushirikiano pamoja na kituo cha televisheni cha Marekani-ABC- na kile cha Uengereza, BBC.Wananchi 1554 wa Afghanistan wameulizwa maoni yao na majibu waliyotoa yanabainisha mabadiliko makubwa katika mtazamo wao kuelekea mustakbal wa nchi yao.

Kwa mtazamo wa kijuu juu, mtu anashindwa kuamini matokeo ya uchunguzi huo wa maoni ya umma. Licha ya visa vya matumizi ya nguvu visivyokwisha, licha ya umaskini na rushwa, kwa mara ya kwanza kabisa idadi kubwa ya wananchi wa Afghanistan wanaangalia kwa jicho jema mustakbal wa nchi yao. Katika utafiti mpya wa maoni ulioongozwa na kituo cha matangazo cha Ujerumani ARD na washirika wake wa ABC na BBC, asili mia 70 ya walioulizwa maoni yao wamejibu wanahisi nchi yao inafuata njia inayofaa. Idadi hiyo imeongezeka kwa asili mia 30 ikilinganishwa na utafiti wa maoni kama huo uliofanyika mwaka mmoja uliopita.

Hali hiyo ya matumaini hailingani na mtazamo wa Marekani na nchi za Ulaya ambako viongozi wanahisi hali si nzuri hivyo nchini Afghanistan. Lakini masuala waliyoulizwa Waafghanistan zaidi ya 1500 yametoa angalao sababu tatu zinazonyesha kwanini Waafghani wanajiwekea matumaini mema namna hiyo. Sababu ya kwanza inatokana na uchaguzi uliopita wa rais. Katika wakati ambapo walimwengu walijishughulisha zaidi na madai ya udanganyiifu wakati wa uchaguzi, Waafghanistan wao walishusha pumzi kuona kwamba uchaguzi huo, ambao hapo awali Wataliban walitishia kuufuja kwa matumizi ya nguvu na vitisho, umepita salama tena bila ya kuchochea vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Asili mia 75 ya walioulizwa maoni yao wameridhika na jinsi uchaguzi huo ulivyopita-hata kama ni wachache tuu wanaohisi kwamba uchaguzi huo umefanyika kama inavyostahiki.

Sababu ya pili inatokana na kuanza kuimarika mahitaji ya kila siku ya kimaisha. Katika maeneo mengi, wananchi wanaanza hivi sasa kujipatia umeme. Hali hiyo inawasaidia wengi wanaotaka kufungua shughuli ndogo ndogo za kibiashara, inabuni nafasi za kazi na kuwafanya Waafghanistan wengi wawe na matumaini mema ya kimaisha kwa siku za mbele. Na hatimae watu wanazidi kujiwekea matumaini kwamba hata vita dhidi ya Wataliban na makundi mengine ya waasi, kuna siku vitakwisha tuu. Hisia hizo zinapingana na zile za mwaka mmoja uliopita ambapo ilionekana kana kwamba Wataliban ndio wenye nguvu kabisa nchini humo.

Sababu hizo zinawafanya wanajeshi wa kigeni wasiangaliwe tena kwa jicho jema nchini humo. Asili mia 40 ya Waafghanistan hawauangalii kwa jicho jema mchango wa wanajeshi wa Marekani na wale wa jumuia ya kujihami ya magharibi NATO nchini humo. Kiroja, hata hivyo, ni kwamba Waafghanistan wanaunga mkono kwa wingi mkakati mpya wa rais Obama kuelekea nchi yao.

Kama ilivyokua katika miaka ya nyuma, na safari hii pia maoni yanatofautiana toka jimbo moja hadi jengine la Afghanistan. Hata hivyo, katika maeneo ambako matumizi ya nguvu yanaendelea, mfano Kandahar, wananchi wameanza kujiwekea matumaini katika wakati ambapo katika eneo la Helmand bado wananchi hawaoni ishara yoyote ya matumaini.

Mwandishi: Henze, Arnd/Hamidou, Oummilkheir/ZR

Mhariri: Miraji Othman