China inaendesha kambi za vizuizi mjini Xinjiang
24 Septemba 2020Taasisi ya ASPI imesema imebaini zaidi ya vituo 380 vinavyoshukiwa kuwa vizuizi katika mkoa huo, ambako China inaaminika kuwashikilia zaidi ya wafungwa milioni moja wa jamii ya Uighur na wakaazi wengine Waislam wanaozungumza Kituruki. Idadi ya vituo hivyo ni kubwa kwa asilimia 40 kuliko idadi iliyokadiriwa awali, umesema utafiti huo na kwamba vituo hivyo vimekuwa vikiongezeka licha ya madai ya China kwamba Waighur wengi wameachiwa huru.
Kwa kutumia picha za satelaiti, ripoti za vyombo vya habari, mashuhuda na nyaraka rasmi za ujenzi, taasisi hiyo imesema angalau vituo 61 vimeshuhudia shughuli za upanuzi na ujenzi kati ya mwezi Julai 2019 hadi Julai mwaka huu. Vituo 14 zaidi navyo vimekuwa vikijengwa mwaka huu na karibu vituo 70 vimeondolewa uzio au ukuta kudhihirisha kuwa matumizi yake yamebadilishwa au vimefungwa.
China kwa mara nyingine, imekana madai hayo ya kuwepo na vituo vya vizuizi. Serikali inasema vituo hivyo ni kwa ajili ya mafunzo ya kiufundi na kutumiwa katika kukabiliana na ugaidi. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje, Wang Wenbin ameuelezea utafiti wa ASPI kuwa wa kutiliwa mashaka.
''Hakujawahi kuwepo na kambi zinazojulikana kama vizuizi huko Xinjiang. Mara kadhaa tumejibu ripoti zinazohusiana na China zilizotungwa na Taasisi ya mikakati ya sera ya Australia (ASPI)".
Hayo yakijiri China imewazuia wanazuoni wawili wa Australia kuingia nchini humo ikiwa ni hatua ya kulipiza kisasi iliyochukuliwa na Australia mapema mwaka huu ya kufuta visa za maafisa wawili wa China. Mmoja wa wanazuoni hao ni mtafiti Alexander Joske kutoka taasisi ya ASPI iliyochapisha utafiti wa leo pamoja na Profesa Clive Hamilton wa Chuo Kikuu cha Charles Sturt mjini Canberra. Haijajulikana wazi ikiwa wanazuoni hao walikuwa wamepanga kuitembelea China hivi karibuni.
Mwezi Desemba mwaka jana, gavana wa mji wa Xinjiang Shohrat Zakir alisema watu wote waliokuwa wakipatiwa mafunzo katika vituo mjini humo walihitimu masomo na kupata ajira. Lakini makundi ya haki za binadamu yanadai kuwa mamlaka zimekuwa zikiwaingiza watu viwandani na kuwatumikisha. Sera za China mjini Xinjiang zimekosolewa kimataifa huku kukiwa na wito wa Umoja wa Mataifa kufanya uchunguzi.
Hata hivyo, China inatetea sera zake za mjini Xinjiang ambako inasema programu za mafunzo, mifumo ya kazi na elimu bora inamaanisha kuwa maisha yameboreshwa.