1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utabiri wa Pele kuhusu Afrika utatimia lini?

26 Mei 2014

Nguli wa soka ulimwenguni, Pele alitabiri nchi mojawapo ya Afrika kuchukua kombe la dunia kabla ya karne ya 20 haijamalizika. Matumaini ya mashabiki wa soka barani Afrika yapo mikononi mwa nchi tano

https://p.dw.com/p/1C7EB
Brasilianische Fußballstars (Bildergalerie)
Picha: picture-alliance/KPA

Nchi tano zitakazoliwakilisha bara la Afrika mara hii katika dimba la Kombe la Dunia ni Algeria, Cameroon, Ghana, Ivory Coast na Nigeria. Ni kocha mmoja tu kati ya timu hizo za taifa ambaye ameshaweka bayana matumaini ya kusonga mbele na hatimaye kuchukua ubingwa huo wa dunia naye ni Kwesi Appiah wa Ghana (Black Stars).

"Timu nzuri ni ile inayojivunia uwezo wake ilionao" alisema Appiah ambaye anasema Ghana ina kikosi imara hivyo anaamini itasonga mbele na hatimaye kuchukua kombe la dunia.

Maneno hayo ya Kwesi Appiah yanaweza yakawashangaza baadhi ya mashabiki wa soka kutokana na ugumu wa kundi la Black Stars ambalo linajumuisha Ujerumani, Ureno na Marekani iliyocheza nayo katika mzunguko wa pili wa kombe la dunia lililopita nchini Afrika kusini.

Flash-Galerie Fußball WM 2010 Südafrika Viertelfinale Uruguay vs Ghana
Asamoah Gyan alikosa kufunga penalti ambayo ingeipa Ghana tikiti ya kucheza nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka wa 2010Picha: AP

Kutokana na ugumu wa kundi hilo, wachambuzi wengi wa soka hawaipi nafasi Ghana kuvuka hatua ya kwanza ya michuano hiyo kama ilivyofanya katika michuano iliyopita ambapo kama sio Luis Suarez kushika mpira uliokuwa unaenda wavuni na kisha Asamoah Gyan kukosa tuta, basi Ghana ingekuwa nchi ya kwanza kutoka Afrika kutinga katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa ya kandanda duniani.

Ukiachilia mbali nchi za Afrika kushindwa kufika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo, lakini pia zina matoke mabovu katika hatua ya makundi kwenda hatua ya mtoano kwani hadi sasa hakuna zaidi ya mataifa mawili ya Afrika yaliyoweza kusonga mbele katika hatua ya makundi hali ambayo inadhihirisha udhaifu wa timu kutoka bara hilo.

Mchezaji nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza na Liverpool, John Barnes amezitaka nchi za Afrika kuwa na fikra chanya ili ziweze kuishangaza dunia katika michuano hiyo.

Didier Drogba anafahamu kuwa hii ni fursa yake ya mwisho kuiwakilisha nchi yake katika Kombe la Dunia
Didier Drogba anafahamu kuwa hii ni fursa yake ya mwisho kuiwakilisha nchi yake katika Kombe la DuniaPicha: Getty Images

"Waafrika wanatakiwa kuonesha uchu na nidhamu wakati wanazichezea nchi zao kama vile wanavyokuwa katika klabu zao za ulaya" alisema Barnes wakati akiongea na kituo cha televisheni cha Afrika Kusini cha Supersport.

Lakini Barnes ambaye ameichezea Uingereza katika fainali mbili za dunia ya mwaka 1986 na 1990, uongozi mbovu wa soka Afrika unachangia kuharibu vipaji vya wachezaji wa soka wa Afrika kama ilivyokuwa kwa Samuel Eto'o wa Cameroun na Emannuel Adebayor ambao mara kadhaa walikuwa wanaingia matatani na vyama vya soka vya nchi zao.

"Tatizo kubwa lililopo Afrika ni viongozi wetu ambao hawatuheshimu sisi" alisema Eto'o wakati akiongea na mtandao wa Shirikisho la soka Afrika CAF. Mchezaji nyota wa zamani wa Liberia, George Weah ambaye ndiye mchezaji pekee kutoka Afrika kuwa mchezaji bora wa dunia, Ulaya na Afrika, anakiri kuwepo kwa changamoto hiyo ya uongozi wa soka Afrika.

"Wachezaji wa zamani ndio wanaoongoza soka la ulaya wakati wale wasio na mapenzi na uwezo wa mchezo ndio wanaotawala Afrika" alisema Weah. Kocha wa Algeria ambaye ni raia wa Bosnia Vahid Halilhodzic amelaumu siasa kuingilia mchezo wa soka Afrika, lakini pia mazingira ya kiuchumi ambayo yanachangia kutokuleta mafanikio katika kombe la dunia.

FIFA Präsident Sepp Blatter und Vizepräsident Issa Hayatou
Rais wa FIFA Sepp Blatter na Rais wa CAF Issa HayatouPicha: picture-alliance/dpa

"Soka la kimataifa ni maarufu sana Afrika na baadhi ya wanasiasa wanatumia mchezo huu kujipatia umaarufu, wanauingilia na kuleta migongano katika vyama" alisema Halilhodzic.

Rais wa Shirikisho la Soka Afrika CAF, Issa Hayatou ambaye ni raia wa Cameroon, anaamini mwaka 2014 utakuwa ndio mwanzo wa nchi za Afrika kupata matokeo mazuri katika fainali za dunia. "Sioni kwanini Afrika haiwezi ikawa na mwakilishi mmoja au wawili katika hatua ya nusu fainali au hata fainali" alisema Hayatou wakati akiongea na mtandao wa CAF.

Vyovyote itakavyokuwa kama utabiri wa Pele utafanikiwa au ndoto ya Kwesi Appiah ya Ghana kutwaa kombe la dunia mwaka huu, lakini ukweli unabaki pale pale kuwa mashabiki wa soka kutoka bara la Afrika lenye raia karibu billioni moja wanasubiri kwa shauku kubwa kuona mwakilishi wao akitwaa kombe hilo lenye heshima kubwa zaidi duniani kuliko michuano yoyote ile kwa upande wa mpira wa miguu.

Mwandishi Anuary Mkama/AFP
Mhariri: Bruce Amani