Usitishaji wa mapigano kati ya Israel na Hezbollah waanza
27 Novemba 2024Wakaazi wameonekana wakisafiri kwenye magari yaliyojaa mali zao kurudi kusini mwa Lebanon licha ya onyo kutoka kwa wanajeshi wa Israel na Lebanon kwamba wasikae kwenye maeneo fulani. Kama utaheshimiwa kikamilifu, utafikisha mwisho karibu miezi 14 ya mapigano kati ya Israel na Hezbollah. Mpango huo uliosimamiwa na Marekani na Ufaransa, na kuidhinishwa jana jioni na Israel. Emmanuel Macron ni Rais wa Ufaransa. Makubaliano hayo yanatoa wito wa kusitishwa mapigano kwa miezi miwili kwanza na unawahitaji Hezbollah kusitisha uwepo wao kusini mwa Lebanon, wakati askari wa Israel wakirejea kwenye upande wao wa mpaka. Maelfu ya askari wa ziada wa Lebanon na walinda amani wa Umoja wa Mataifa watapelekwa kusini, na jopo la kimataifa linaloongozwa na Marekani litafuatilia utekelezaji huo. Viongozi mbalimbali wa dunia wamepongeza makubaliano hayo wakitoa wito wa kutekelezwa kikamilifu. Naye afisa wa Hamas Sami Abu Zuhri ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa kufuatia makubaliano hayo ya Israel na Hezbollah, Hamas pia wako tayari kusitisha vita na Israel.