Ushindi wa upinzani Poland
22 Oktoba 2007Kwanza ni gazeti la “Augsburger Allgemeine”:
“Wapoland wengi bila shaka walifarajika baada ya uchaguzi wa jana. Pia majirani na washirika wa Poland katika Umoja wa Ulaya wanaweza kufarajika. Iwe ni kwenye majadiliano juu ya mkataba wa Ulaya, kuhusu ushirikiano mpya na Urusi au kwenye mvutano juu ya kuwepo kwa siku dhidi ya adhabu ya kifo – popote serikali ya Poland chini ya waziri mkuu Jaroslaw Kaczynski iliyazuia mambo yaendelee. Wakati huo huo Poland ni mpokeaji mkubwa zaidi wa msaada wa Umoja wa Ulaya.”
Mhariri wa “Thüringer Allgemeine” vilevile anaangalia mahusiano kati ya Poland na Umoja wa Ulaya na amechambua hivi matokeo ya uchaguzi:
“Bado Poland inaweza ikajumuishwa katika Umoja huu. Wanasiasa walioko Brussels au Berlin walishikilia wazo la Umoja wa Ulaya katika wiki ngumu zilizopita na walitumai kwamba waziri mkuu Kaczynski atashindwa kwenye siku ya uchaguzi. Basi, angalau mmoja wa mapacha Kacyznski ameangushwa madarakani. Waziri mkuu huyu Jaroslaw Kaczynski hakuweza kuwashawishi wananchi wenzake na sera za kizalendo na za kikanisa. Pacha wake Lech lakini anabakia madarakani. Katika siku za usoni, atajaribu kila awezalo kujitambulisha kama mwokozi na mtetezi wa maslahi ya Poland.”
Mada nyingine inayogonga vichwa vya habari hii leo ni mvutano kati ya Iraq na Uturuki juu ya suala la Wakurdi huko Kaskazini mwa Iraq. Ufuatao ni uchambuzi wa gazeti la “Badische Zeitung”:
“Iraq huenda ikakumbwa na hata vita vingine. Iwapo Waturuki watalivamia eneo la Wakurdi Kaskazini mwa Iraq, tatizo hilo halitatatuliwa, bali watasababisha tatizo jingine kubwa. Usalama wa eneo zima la Mashariki ya Kati utaathirika zaidi. Suala la Wakurdi ambao wanataka kujitegemea na kujitenga na Uturuki na Iraq linabidi litatuliwe kwa njia ya kisiasa. Tangu miaka mingi, Wakurdi waliachwa kando au hata waliaibidhwa na serikali ya Saddam Hussein na vilevile ile ya Uturuki. Kuna hospitali na shule chache sana, kumbe kwa muda mrefu eneo hili lilikuwa katika hali ya dharura.”
Ni gazeti la “Berliner Zeitung”. Mhariri wa “Berliner Morgenpost” anaangalia upande wa waasi Wakurdi wa PKK baada ya wao kulishambulia jeshi la Uturuki na kuwaua wanajeshi 12. Nia yao basi ni ipi? Gazeti limeandika:
“Waasi wanataka mizozo iwe mikali zaidi ili wananchi wenzao waamini kuwa mapigano ni njia ya pekee. Iwapo serikali husika itachukua hatua ya kijeshi na kuwakomesha waasi, hilo litasababisha waasi kujipatia wafuasi wengi.”
Na la mwisho ni gazeti la “Westdeutsche Zeitung” juu ya mvutano huu ambao unaihusu pia Marekani. Tunasoma kuwa:
“Mzozo kati ya Uturuki na Marekani ni mbaya sana kwa pande zote mbili. Jeshi la Marekani linategemea vituo vyake nchini Uturuki na haki ya kutumia anga ya Uturuki. Bila ya hayo, Marekani itapata shida kubwa katika operesheni zake huko Iraq na Afghanistan. Uturuki, kwa upande wake, haiwezi kupinga kabisa maslahi ya nchi za Magharibi. Kisa hicho ni kama mtihani kwa Uturuki katika juhudi zake za kujiunga na Umoja wa Ulaya.”