1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usalama wazidi kuzorota Libya

28 Julai 2014

Kiasi ya watu 150 wameuawa katika ghasia ambazo zimezuka upya katika miji ya Benghazi na Tripoli katika kipindi cha wiki mbili zilizopita kufuatia makabiliano makali kati ya wanajeshi na makundi hasimu ya wanamgambo.

https://p.dw.com/p/1CjkB
Picha: Reuters

Wizara ya afya ya Libya imesema tangu makabiliano hayo kuzuka wiki mbili zilizopita, kiasi ya watu 94 wameuawa katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli na zaidi ya wengine 400 wamejeruhiwa wakati wa mapambano kati ya wanajeshi na wanamgambo wanaong'angania kuudhibiti mji huo.

Kiasi ya wengine 55,wengi wao raia wameuawa katika mji wa Benghazi mwishoni mwa juma katika makabaliano mengine kati ya jeshi na makundi ya wanamgambo wa kiislamu.

Maroketi yalenga mapipa ya mafuta

Shirika la taifa la mafuta limesema maroketi yaliyokuwa yakirushwa, yalilenga matangi ya kuhifadhia mafuta karibu na uwanja wa ndege wa Tripoli hapo jana na kusababisha moto mkubwa ambao wazima moto wameshindwa kuuzima. Matangi hayo yalikuwa yanahifadhi kiasi cha lita milioni sita za petroli na yako karibu na mengine yanayohifadhi gesi na diesel.

Abiria wakisubiri kusafiri katika uwanja wa ndege wa Miitiga
Abiria wakisubiri kusafiri katika uwanja wa ndege wa MiitigaPicha: Reuters

Wizara ya mafuta na nishati imewaonya raia wanaoishi karibu na maeneo ya matangi hayo kuondoka mara moja kuepusha majanga ya kibinadamu na kimazingira kufuatia kuzuka kwa moto huo mkubwa.

Mapigano hayo ya wiki mbili ndiyo mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo tangu kung'olewa na baadaye kuuuawa kwa aliyekuwa kiongozi wa tafa hilo Muammar Gaddafi mwaka 2011.

Marekani,Umoja wa Mataifa na Uturuki zimewaondoa wafanyakazi wa balozi zao kutoka taifa hilo la kaskazini mwa Afrika. Marekani iliwahamishia wafanyakazi hao katika nchi jirani ya Tunisia siku ya Jumamosi chini ya ulinzi mkali baada ya mapigano kupamba moto karibu na ubalozi wake mjini Tripoli.

Msafara wa magari yaliyokuwa yamewabeba maafisa wa Uingereza ulishambuliwa jana katika jaribio la utekaji nyara nje ya mji wa Tripoli ulipokuwa ukielekea Tunisia na ingawa hakuna mtu aliyejeruhiwa katika kisa hicho, magari yaliharibiwa.

Wajumbe maalumu wa jumuiya ya nchi za kiarabu kuhusu Libya,Marekani na umoja wa Ulaya wameelezea wasiwasi wao kuhusu hali inavyozidi kuzorota nchini Libya na kusema hali hiyo imefikia hatua ngumu na kutaka mapigano kusitishwa mara moja.

Nchi za magharibi zawataka raia wake kuondoka

Ujerumani, Uingereza ,Ufaransa, Uholanzi, Ubelgiji, Misri na Uturuki nimiongoni mwa nchi nyingine ambazo zimewataka raia wao walioko Libya kuondoka nchini humo mara moja kwa sababu ya kudorora kwa hali ya usalama.

Wapiganaji wa kundi la wanamgambo la Misrata
Wapiganaji wa kundi la wanamgambo la MisrataPicha: picture-alliance/AP Photo

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier amesema raia wa Ujerumani walioko Libya wako katika hatari kubwa ya kutekwa nyara na kuuawa kwa sababu sio rahisi kutabiri hali nchini humo itachukua mkondo gani.

Bunge jipya la Libya lililochaguliwa mwezi Juni mwaka huu linatarajiwa na nchi za magharibi kuwa litaweza kumaliza mzozo huo kwa kufikiana makubaliano ya kisiasa wakati wabunge watakapokutana kwa kikao cha kwanza mwezi ujao.

Miaka mitatu baada ya kung'olewa kwa Gaddafi,ndoto ya Libya kuifikia demokrasia imezongwa na malumbano ya wenyewe kwa wenyewe ya kisiasa na mapigano ya mara kwa mara kati ya makundi hasimu ya waasi waliosaidia kumuondoa Gadafi madarakani ambayo yanataka kuidhibiti miji mikuu na viwanda vya mafuta.

Mwandishi:Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Gakuba Daniel