1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usalama waimarishwa Iraq

3 Novemba 2014

Iraq imeimarisha usalama huku kukiwa na hofu ya kundi la Dola la Kiislamu kufanya mashambulizi makubwa wakati Waishia Jumatatu (03.11.2014) wakikusanyika katika mji wa Karbala.

https://p.dw.com/p/1DgFG
Kikosi cha Iraq kusini mwa nchi hiyo.
Kikosi cha Iraq kusini mwa nchi hiyo.Picha: Reuters

Kundi la Dola la Kiislamu limedai kuhusika na miripuko miwili ya mabomu dhidi ya mahujaji wa Kishia ambayo imesababisha watu 23 kuuwawa mjini Baghdad hapo jana.

Katika taarifa iliowekwa kwenye mtandao jana usiku kundi hilo limesema mashambulizi hayo ya mabomu yaliotegwa kwenye magari yamefanyika licha ya hatua kali za usalama zilizochukuwa wakati huu wa kumbukumbu ya tukio kuu ya wale iliowaita watu wasiokuwa na dini.

Mashambulizi hayo mawili hapo jana yaliwalenga mahujaji wa Kishia na mahema yalioko barabarani yaliokuwa yakiwahudumia watu wanaoelekea katika mji mtakatifu wa Karbala kwa ajili ya siku kuu ya kidini ya Ashura.

Ziara hizo za hija ni shabaha kuu ya mashambulizi kwa wapiganaji wa jihadi wa kundi la Dola la Kiislamu ambao walifanya mfululizo wa mauaji makubwa katika siku za hivi karibuni na kuuwa watu wengi wa kabila moja katika jimbo la magharibi mwa Iraq la Anbar.

Ziara hizi za hija zimekuwa zikishambuliwa kabla wakati wa sikukuu ya Ashura lakini kumbukumbu za mwaka huu zinakabiliwa na hatari kubwa zaidi baada ya kundi la Dola la Kiislamu kuteka sehemu kubwa ya ardhi ya Iraq hkatika shambulio lao la mwezi wa Juni.

Usalama waimarishwa

Serikali imewamwaga maelfu ya askari wa usalama wakisaidiwa na wanamgambo kuwalinda mahujaji kwa kile kitakachokuwa mtihani wa kwanza mkuu wa serikali mpya inayoongozwa na Waziri Mkuu Haidar al-Abadi.

Msikiti wa Hussein mjini Karbala.
Msikiti wa Hussein mjini Karbala.Picha: AFP/Getty Images/M. Sawaf

Polisi wamewekwa kwenye vitongoji vyote vya Washia vilioko Baghdad na vikosi vya usalama vinalinda barabara ya kilomita 100 kutoka mji mkuu kuelekea Karbala.

Luteni Generali Othman al - Ghanimi amewaambia waandishi wa habari kwamba mjini Karbala zaidi ya askari wa usalama 26,000 wamewekwa wakisaidiwa na helikopta zenye kutowa msaada wa anga na kuchunguza maeneo ya jangwani.

Kundi la IS laendelea kushambuliwa

Muungano wa mataifa ya magharibi na Kiarabu yakiongozwa na Marekani umefanya mashambulizi kadhaa dhidi ya maeneo yanayodhibitiwa na kundi la Dola la Kiislamu nchini Iraq na Syria huku Canada ikifanya shambulio lake la kwanza dhidi ya kundi hilo hapo jana.

Kikosi cha mizinga cha Iraq.
Kikosi cha mizinga cha Iraq.Picha: Reuters/Stringer

Ndege za Canada chapa CF -18 zilifanya mashambulizi kwenye mji wa Fallujah wakati wizara ya ulinzi ya Marekani ikisema ndege yake imefanya mashambulizi matano hapo Jumamosi na Jumapili karibu na mpaka wa Syria wa mji wa Kobane.

Wanamgambo wa Kikurdi wamekuwa wakijihami dhidi ya shambulio la kundi la IS katika mji huo tokea takriban wiki saba na wameongezewa nguvu mwishoni mwa wiki kutokana na kuwasili kwa wapiganaji 150 wa kikosi cha Peshmerga cha Wakurdi wa Iraq wakiwa na silaha nzito.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman