1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usalama wa vinu vya nyuklia Japan

13 Machi 2011

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amekutana kwa dharura na baadhi ya mawaziri wake kutokana na hali ya wasiwasi juu ya usalama wa vinu vya kinyukliya vya Japan.

https://p.dw.com/p/10YUc
Kinu nambari 1 cha FukushimaPicha: dapd

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani jana jioni alifanya mkutano wa dharura pamoja na baadhi ya mawaziri wake, wakiwemo wale wa mazingira, mambo ya kigeni na wa mambo ya ndani. Walizingatia namna Ujerumani itakavoweza kuisadia Japan kukabiliana na matokeo ya mtetemeko mkubwa wa ardhi uliotokea katika nchi hiyo, na pia mawimbi ya Tsunami yalioleta uharibifu mkubwa. Mada ya mazungumzo ilihusu pia hatari zinazotokana na kinu cha kinyukliya kinapoharibika, ambapo jambo linalofuata linaweza kuwa ni kitisho cha kuyayuka nguvu yenyewe ya atomiki.

Pressekonferenz Merkel Japan Flut Atomkraftwerk Explosion
Kansela Angela Merkel, na waziri wa mambo ya kigeni Guido Westerwelle.Picha: dapd

Ujerumani yaijadili Japan

Balaa lililotokea katika kinu cha kinyukliya cha Fukushima huko Japan ni la ukubwa gani? Pia serekali ya Ujerumani hadi jana jioni ilikuwa katika kiza. Katika mkutano huo wa dharura, Kansela Angela Merkel alionekana kuwa na wasiwasi, na kwamba uwezekano wa kuyayuka mafuta ya kinyukliya katika kinu hicho kilichoharibika ni jambo la kutia wasiwasi na lisilokuwa la kawaida. Hali hiyo inaweza ikabakia na athari katika uendeshaji wa vinu vya kinyukliya vya hapa Ujerumani. Bibi Merkel alitangaza kwamba kutafanywa uchunguzi juu ya viwango vya usalama katika vinu vya Ujerumani.

Bibi Merkel alisema serekali ya Ujerumani imeiahidi serekali ya Japan kila aina ya misaada, na kwamba hatua thabiti zimeshachukuliwa, kama alivosema waziri wa mambo ya kigeni, Guido Westerwelle kuwa serikali imewapelekea wananchi wa Japan sio tu pole na hisia zao, lakini wameisadia. Tayari wafanya kazi wa shirika la Ujerumani la kutoa misaada ya dharura ya kiufundi wako Japan, na wengine 40 wako njiani wakielekea huko.

Japan Erdbeben Tsunami
Athari ya tsunami katika eneo la Kesennuma Miyagi, Kaskazini mwa Japan.Picha: dapd

Shughuli za uokozi

Watu hao, wakisaidiwa na mbwa, watawatafuta na kuwatoa watu waliofukiwa chini ya vifusi vya madongo yaliotokana na kuanguka majumba katika miji. Kansela Merkel pia alitangaza kwamba tayari mabingwa juu ya usalama wa vinu vya kinyukliya wako tayari kusafiri hadi Japan. Kansela alijaribu kuondoa wasiwasi juu ya hatari yeyote kwa Ujerumani kutokana na ajali hiyo.

Vyama vya upinzani na wapinzani wa nishati ya kinyukliya, kutokana na maafa haya yaliojiri huko Japan, wanajihisi wamepata nguvu katika hoja zao. Kiongozi wa wabunge wa Chama cha Kijani hapa Ujerumani, Jürgen Trittin, aliyalaumu yale mapatano yaliofikiwa na vyama vya CDU/CSU na FDP vinavounda serekali ya mseto ya mjini Berlin kurefusha muda wa kufanya kazi vinu vya kinyukliya vya hapa Ujerumani.

Jana mjini Stuttgart, maelfu ya Wajerumani walikwenda mabarabarani wakiandamana kupinga matumizi ya nishati ya kinyukliya. Kwa sasa Kansela Merkel anapinga mijadala kuhusu suala la vinu vya kinyukliya vya Ujerumani. Lakini Bib Merkel huyo huyo ametangaza kwamba kile kitakachoweza kusomwa na watu kutokana na ajali hiyo ya Japan kitakuwa na matokeo yake pia hapa Ujerumani.

Mwandishi: Fuchs, Richard/ Othman, Miraji/ZR
Mhariri: Mohammed Dahman