1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Fujo za wahuni zagubika Euro 2016

15 Juni 2016

Shambulio la kigaidi mjini Paris, na fujo za wahuni katika fainali za kombe la mataifa ya Ulaya Euro 2016 nchini Ufaransa na kitisho cha vita baridi barani Ulaya ni miongoni mwa mada magazetini

https://p.dw.com/p/1J6qS
Migomo ya wanaopinga mageuzi ya sheria za kazi mjini ParisPicha: Reuters/J. Naegelen

Tuanzie lakini Paris na shambulio la kigaidi lililoangamiza maisha ya askari polisi na mkewe. Gazeti la "Emder Zeitung" linaandika:"Kwa mara nyengine tena mwanajihadi amejipa haki ya kuamua kuhusu hatima ya maisha ya mtu mwengine. Hilo pekee ni tusi kwa dini yoyote ile na dhambi pia. Mauwaji hayo yanabainisha kizungumkuti kinachozikaba nchi nyingi za magharibi. Kwasababu wengi kati ya washambuliaji baadhi ya wakati wanakuwa tayari wanajulikana na polisi,ila wanapoanza kufuata itikadi kali,mara nyingi hakuna anaekuwa anajua. Wanafanya hivyo kimya kimya. Kijuu juu hakuna anaeweza kuwatambua. Ingawa wengi wanapiga kelele na kudai shughuli za upelelezi ziimarishwe,pamoja na uchunguzi na hatua nyengine za aina hiyo ili kuepusha mashambulio yasitokee, lakini yote hayo hayajasaidia kitu. Na hasa Ufaransa imezidisha makali miaka ya hivi karibu katika shughuli za ulinzi na ukaguzi. Mataifa ya magharibi yanabidi yaachane na fikra kwamba kila kitu kinaweza kueleweka kuambatana na vipimo vyao.

Mashambulio na fujo za wahuni zatishia Euro 2016

Kitisho cha mashambulio ya kigaidi pamoja na fujo za mashabiki wahuni -yote hayo yanatishia mashindano ya fainali za kombe la mataifa barani Ulaya Euro 2016. Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linaandika:"Patahitajika miujiza kutokea ili nchi hiyo iishi wiki nne za furaha na shangwe, kipa umbele kikiwa dimba tu. Matumaini hayo yalififia masaa machache tu baada ya fainali hizo kuanza,pale mashabiki wa Uingereza na Urusi walipopigana majiani mjini Marseille kwa namna ambayo timu zao sasa zinakabiliwa na kitisho cha kuzuwiliwa kucheza fainali za Euro 2016. Hilo pekee limebainisha kwamba waandalizi nchini Ufaransa wamezidiwa.

Kwasababu polisi walioandaliwa makusudi kwaajili ya kupambana na machafuko,wamekawia kuingilia kati na walikuwa dhaifu. Mfumo jumla wa usalama wakati huu wa fainali za kombe la mataifa barani Ulaya unawekewa suala la kuuliza hivi sasa. Kuna zaidi ya hayo pia,nchi ambayo ndio miezi sita tu iliyopita ilikuwa shabaha ya mashambulio makubwa ya kigaidi,haiwezi wakati huo huo kuwadhibiti kikamilifu wahuni wafanyafujo,vuguvugu la wafuasi wa mrengo wa kushoto wanaoandamana na kupigana na wakati huo huo kudhamini usalama wa mamilioni ya mashabiki.

Kitisho cha kuibuka upya vita baridi duniani

Mada yetu ya mwisho inahusiana na kitisho cha kurejea upya enzi za vita baridi barani Ulaya.Gazeti la "Landeszeitung" linaandika:" Hebu fikiria,vita baridi vimemalizika lakini wewe bado unabidi uendele kulitumikia jeshi. Sawa na ilivyokuwa wakati wa vita baridi na wakati huu pia kuna maamuzi yanayopitishwa na ambayo yanaweza kuwa ya hatari. Katika wakati ambapo jumuia ya kujihami ya NATO inataka kupandisha bendera katika nchi za Balitik,Putin anaamuru zidurusiwe nguvu za jeshi la Urus. Ujumbe ambao NATO inataka kutoa, Kremlin yaonyesha haijauelewa. Kimsingi katika mchezo huu wa kupimana nguvu nchi za magharibi zilitaka kuizuwia Urusi isijibwage katika opereshini nyengine hatari za kijeshi. Lakini hatari ni kubwa sasa kuviona vifaru vya NATO vitakavyowekwa karibu na mipaka ya Urusi vikisababisha mchezo hatari zaidi wa kijeshi.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Iddi Ssessanga