1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Usalama wa mitambo ya nyuklia watiwa shakani upya

16 Julai 2009

Wito wa kuivunja serikali katika jimbo la Schleswig-Holstein, mvutano kati ya familia zinazomiliki makampuni ya magari ya Volkswagen na Porsche ni baadhi ya mada zilizoshughulikiwa na magazeti ya Ujerumani leo Alkhamisi.

https://p.dw.com/p/Iqvy

Lakini tuataanza na ripoti iliyozusha mabishano mapya kuhusu taka zinazotoka kwenye mitambo ya nyuklia.Gazeti la DER NEUE TAG kutoka Wieden linasema:

"Nchini Ujerumani imani ya umma inazidi kupunguka kuhusu usalama wa nishati ya nyuklia baada ya kasoro kadhaa kugunduliwa Julai 4 kwenye mtambo wa nyuklia wa Krümmel. Hata ripoti zilizosema kuwa vyuma vyenye taka za nyuklia, vimevuja majimaji katika mgodi wa zamani wa Asse, kulikozikwa hizo taka za kinyuklia, zimewafanya wananchi kuuliza ikiwa mitambo ya nyuklia kweli ni salama na haichafui mazingira. Hiyo bila shaka ni mada isiyoweza kuepukwa na wanasiasa, kwani Ujerumani inajitayarisha kwa uchaguzi mkuu Septemba ijayo."

Kwa maoni ya gazeti la NORDKURIER, ajali mbali mbali zilizotokea katika mtambo wa nyuklia wa Krümmel zimekitumbukiza chama cha CDU kinachounga mkono nishati ya nyuklia katika hali ngumu na kuongezea:

"Waziri Mkuu wa jimbo la Niedersachsen, Christian Wulff, hakuwa na jingine isipokuwa kukiri kuwa hana hakika iwapo mtambo huo utaweza kuruhusiwa kufanya kazi. Matamshi hayo, ni nyimbo tamu kwa chama cha SPD kinachopigania kupunguza idadi ya mitambo ya nyuklia kote Ujerumani."

Sasa tunapindukia mkasa wa jimbo la Schleswig-Holstein ambako serikali ya muungano kati ya chama cha kihafidhina CDU na wasoshalisiti SPD, ipo hatarini baada ya Waziri Mkuu wa jimbo hilo Peter Harry Carstensen kutoa mwito wa kulivunja bunge lake. Gazeti la NEUE OSNABRÜCKER ZEITUNG linasema:

"Wito wa chama cha CDU katika jimbo hilo kuitisha uchaguzi wa mapema si cho chote isipokuwa mbinu iliyozingatiwa kwa makini. Carstensen anatazamia kunufaika kutokana na mazingira mazuri ya chama cha CDU kinachoungwa mkono na umma katika serikali kuu ya mjini Berlin."

Lakini gazeti la FLENSBURGER TAGEBLATT linasema:

"Mwenyekiti na kiongozi wa wabunge wa SPD katika serikali ya jimbo la Schleswig-Holstein, Ralf Stegner alipaswa kuamua tangu mapema, iwapo chama chake kinapenda kuongoza pamoja na CDU au kingependa kuwa upande wa upinzani. Haiwezekani kufanya yote mawili, kama inavyozidi kudhihirika katika serikali ya jimbo hilo. Kwa hivyo uchaguzi mpya ni suluhisho lililo bora kabisa."

Kwa kumalizia uhariri wa magazeti ya Ujerumani, tunatupia jicho mvutano kati ya familia zinazomiliki makampuni mawili ya magari ya Ujerumani Volkswagen na Porsche. Gazeti la FINANCIAL TIMES DEUTSCHLAND linasema:

"Kilichoshuhudiwa tangu majuma kadhaa katika ugomvi wa Volkswagen na Porsche ni makelele,fitina na mbinu chafu. sasa ni bora kwa pande hizo mbili kuumaliza ugomvi huo upesi iwezekanavyo. Kwani nchi ya Ghuba Qatar, ipo tayari kununua hisa katika VW lakini sio kabla ya familia hizo kumaliza ugomvi wao.

Mwandishi: P.Martin/DPA

Mhariri: Miraji Othman