Usajili wa Ronaldo wamuingiza orodha ya wachezaji ghali
11 Julai 2018Ronaldo amesaini mkataba wa miaka minne katika klabu hiyo inayoshiriki ligi ya Italia maarufu kama Serie A. Kuondoka kwake kunahitimisha mafanikio ya miaka 9 aliyoyapata nchini Uhispania na kumuweka mbali na kesi ya ukwepaji kodi ambayo itamgharimu mshambuliaji huyo wa Ureno faini ya zaidi Dola milioni 20.
Katika barua yake ya wazi mchezaji huyo machachari alisema, "Miaka hii yote nilikuwa na Real Madrid na katika mji huu imekuwa ni furaha katika maisha yangu", akiongeza kwamba "nafikiri muda umefika wa kuanza awamu mpya katika maisha yangu na ndio maana nimeiomba klabu yangu kukubali uhamisho wangu. Ninahisi muda umewadia na ninaomba kila mmoja, hususan mashabiki zetu, tafadhali mnielewe."
Rekodi ya magoli Real Madrid
Ronaldo alijiunga na Real Madrid mwaka 2009 akitokea Manchester United na amekuwa mfungaji bora wa klabu hiyo ya Hispania akiwa amepachika jumla ya magoli 451 katika jumla ya mechi 438. Ameisaidia Real Madrid kushinda ligi ya mabingwa (Champions League) misimu minne, ikiishinda Juventus katika fainali za 2017.
Ameweka rekodi ya magoli 120 katika ligi ya mabingwa, 105 kati ya hayo ni tangu alipojiunga na Madrid, ikiwa ni mara 12 zaidi ya Juventus.
Madai ya ukwepaji kodi
Lakini Ronaldo hakufurahishwa na namna mamlaka za mapato zilivyomchukulia nchini Uhispania. Ronaldo, sambamba na wachezaji wengine wa juu katika nchi hiyo wanatuhumiwa kwa ukwepaji wa kodi, ambapo mamlaka zinasema serikali ilipata udanganyifu wa kodi wa yuro milioni 14.7 kati ya mwaka 2011-14.
Ripoti za vyombo vya habari ambazo hazikuthibitishwa mwezi uliopita zilisema kwamba Ronaldo alikubali kulipa faini ya yuro milioni 18.8. Wachezaji wengine waliolengwa na mamlaka za ulipaji kodi za Hispania hivi karibuni ni pamoja na Lionel Messi, Javier Mascherano na Luka Modric. Kocha wa zamani wa Real Madrid Jose Mourinho ambaye sasa yupo katika klabu ya Manchester United pia anachunguzwa.
Usajili wa mshambuliaji huyo umevunja rekodi katika ligi ya Serie A, ambapo Juventus waliiweka miaka miwili iliyopita wakati walipoilipa Napoli yuro milioni 90 kwa ajili ya Gonzalo Higuain. Ronaldo alianza kung'ara katika klabu ya Sporting Lisbon wakati akiwa na miaka 17. Umaarufu wake ulizidi wakati Alex Ferguson alipomleta Manchester United katika msimu wa 2003-04 na kumpatia jezi namba 7 iliyokuwa ikitumiwa na David Beckham aliyekuwa ameondoka klabuni muda mfupi kabla.
Alitumia misimu sita huko England akishinda ubingwa wa ligi mara tatu, ligi ya mabingwa mara moja na kombe la FA moja.
Wachezaji waliovunja rekodi ya usajili
Kwa usajili wa sasa nyota huyo wa Ureno Cristiano Ronaldo ameingia katika orodha ya wachezaji walionunuliwa kwa bei kubwa katika soka. Wafuatao ni wale waliovunja rekodi.
Neymar (PSG)
Alinunuliwa kwa euro milioni 222 kutoka klabu ya Barcelona na kwenda Paris Saint-German ya Ufaransa mwaka 2017.
Kylian Mbappe (PSG)
Mchezaji chipukizi wa Ufaransa Kylian Mbappe amenunuliwa kwa mkopo wa euro milioni 180 kutoka Monaco na kwenda Paris Saint-German PSG.
Ronaldo (Juventus)
Cristiano Ronaldo amechukuliwa kwa euro milioni 112 ametokea Real Madrid anajiunga na Juventus.
Paul Pogba (Manchester United)
Alinunuliwa kwa euro milioni 105 kutoka Juventus kwenda Manchester United mwaka 2016.
Gareth Bale aliuzwa euro milioni 94 kwenda Real Madrid akitokea Tottenham.