Usain Bolt aandikisha historia katika Olimpiki
15 Agosti 2016Bolt ameingia katika kumbukumbu za historia kwa kuwa mwanariadha pekee katika historia ya miaka 120 ya olimpiki, kushinda medali ya dhahabu mara tatu mfululizo katika mashindano ya mbio za mita 100.
Bolt alishinda mara ya kwanza medali ya dhahabu mwaka 2008 mjini Beijing na kisha London mwaka 2012. Mwanariadha huyo wa Jamaica mwenye umri wa miaka 29 amesema anatazamia ushindi mwingine katika mashindano ya mbio za mita 200 na za mita 100 kupokezana vijiti wiki hii ili kumfanya mtu asiyeshaulika.
Nani kama Bolt?
Punde baada ya kushinda, Bolt amewaambia wanahabari kuwa hii ndiyo sababu alishiriki, kuuthibitishia ulimwengu kuwa ndiye mwanariadha bora zaidi na kuongeza amefurahi na anajivunia ushindi wake. Mwanariadha huyo anayeshikilia rekodi ya dunia katika mbio za mita 100 amesema atastaafu baada ya michuano ya ubingwa dunia mwaka 2017.
Maelfu ya watu walimiminika mitaani nchini Jamaica licha ya barabara kujaa tope baada ya mvua kubwa kusherehekea ushindi wa Bolt.
Lakini si Usain Bolt pekee ambaye amevunja rekodi usiku wa kuamkia leo katika mashindano ya olimpiki ya Rio. Mwanariadha wa Afrika Kusini Wayde van Niekerk ameandikia rekodi ya kuzikamilisha mbio za mita 400 kwa muda wa sekunde 43.03 na kujinyakulia medali ya dhahabu.
Van Niekerk amevunja rekodi iliyowekwa na Johnson ya sekunde 43.18 mwaka 1999. Van Niekerk mwenye umri wa miaka 24 aliwaduwaza washindani wake wa karibu Krinadi James wa Grenada aliyemaliza mashidano hayo kwa muda wa sekunde 43.76 na mshindi wa medali ya dhahabu wa mashindano ya olimpiki ya 2008 La Shawn Meritt wa Marekani.
Sumgong aipa Kenya dhahabu ya kwanza Rio
Mkenya Jemima Sumgong amekuwa mwanamke wa kwanza kutoka Kenya kushinda dhahabu katika mbio za masafa marefu katika mashindano ya olimpiki hapo jana.
Katika Tennis, Andy Murray wa Uingereza alimbwaga muargentina Juan Martin del Potro ambaye aliwashinda wachezaji nyota wa Tennis akiwemo mserbia Novak Djokovik na mhispania Rafel Nadal kufika fainali.
Mwanariadha wa Jamaica Elaine Thompson naye aliibuka mshindi wa nishani ya dhahabu upande wa wanawake katika mashindano hayo ya mita 100 siku ya Jumamosi.
Thompson mwenye umri wa miaka 24 alishinda mbio hizo katika muda wa sekunde 10 nukta 71 na kumpiku Fraser Pryce mwanariadha pia wa Jamaica aliekuwa amepania kuandikisha rekodi kama ya Bolt ya kuwa mwanamke wa kwanza kushinda mbio hizo mara tatu mfululizo. Pryce alimaliza wa tatu nyuma ya Towie Bowie kutoka Marekani.
Hii leo michezo inayosubiriwa kwa hamu na ghamu ni fainali za mashindano ya mita 400 kwa wanawake, mashindano ya kuruka vihunzi na maji kwa wanawake na mbio za mita 800 kwa wanaume.
Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa
Mhariri:Iddi Ssessanga