Usafiri waparaganyika Ulaya kutokana na kimbunga Ciara
10 Februari 2020Maeneo ya kaskazini mwa Ufaransa yamewekwa katika tahadhari ya juu ambapo watu wameshauriwa kuepuka kwenda pwani kutokana na uwezekano wa athari za upepo mkali wa kimbunga hicho. Uingereza, ambayo imekumbwa na upepo huo mkali jana Jumapili pamoja na mafuriko makubwa katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo, inaendelea kuwa katika hali ya tahadhari wakati ofisi ya utabiri wa hali ya hewa ikionya kuhusu upepo mkali, mvua kubwa na theluji.
"Wakati kimbunga Ciara kinatoweka, hii haina maana kwamba tunaingia katika kipindi cha utulivu wa hali ya hewa," afisa wa idara ya utabiri wa hali ya hewa Alex Burkill amesema.
Kasi ya juu ya upepo iliyorekodiwa ilikuwa kilometa 150 kwa saa katika kijiji cha kaskazini magharibi mwa Wales cha Aberdaron.
Safari kadhaa za ndege zimefutwa ama kucheleweshwa na makampuni ya safari za treni yamewataka wasafiri kutosafiri na wameruhusu safari chache pamoja na kudhibiti kasi ya mwendo.
Huduma ya feri kati ya Dover kusini mashariki mwa Uingereza na mji wa bandari nchini Ufaransa wa Calais zimesitishwa jana hadi itakapotolewa taarifa nyingine.
Nyumba kadhaa zakosa umeme
Nchini Ireland, ambako tahadhari ilikuwa katika kiwango cha rangi ya chungwa, ambayo haijafikia kiwango cha juu kabisa, kutokana na hatari ya mafuriko katika maeneo ya pwani, nyumba 10,000, mashamba na biashara zimekuwa hazina umeme.
Ubelgiji pia ilikuwa katika tahadhari na kiasi ya safari 60 za ndege kwenda na kutoka Brussels zilifutwa. Katika mji huo, miti na vyuma vinavyotumiwa kusaidia katika ujenzi wa majengo viliondolewa na upepo na baadhi ya majengo kuharibiwa lakini hakuna mtu aliyefariki.
Nchini Ujerumani, huduma za treni za kwenda mbali zilisitishwa. Upepo wa kimbunga ulikuwa mkali sana , na tukalazimika kusitisha kabisa safari za treni za mbali nchini Ujerumani siku ya Jumapili," Msemaji wa shirika la reli nchini Ujerumani Deutsche Bahn, Achim Stauss aliliambia shirika la habari la AFP.
Viwanja kadhaa vya ndege nchini Ujerumani vimelazimika kufuta safari wakati kimbunga hicho kikipita katika eneo la kaskazini. Viwanja vya ndege vya Frankfurt, Munich, Kolon na Hannover vilikuwa miongoni mwa vilivyoathirika, wakati katika uwanja wa Duesseldorf, safari 120 zilifutwa.
Mchezo wa kandanda wa Bundesliga kati ya mahasimu wa jadi Borussia Moenchengladbach dhidi ya FC Kolon umefutwa jana kutokana na hatari ya kimbunga hicho.