1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yadaiwa kukiuka mamlaka ya anga ya Uturuki

Mjahida 6 Oktoba 2015

Ubalozi wa Urusi mjini Ankara, Uturuki umesema unayachunguza madai kuwa moja ya ndege za kivita za Urusi zinazofanya operesheni zake Syria zimekiuka mamlaka ya anga ya Uturuki.

https://p.dw.com/p/1GjGh
Ndege ya kivita ya Urusi
Ndege ya kivita ya UrusiPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Kots

Uturuki imesema ndege za kivita za Urusi zimekiuka anga zake siku ya Jumapili,ikisema hili tayari limesharejewa mara mbili ndani ya siku tatu zilizopita. Uturuki tayari imeuonya ujumbe wa urusi kuwa hatua kama hiyo haipaswi kurejewa tena la sivyo Urusi itawajibishwa.

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu ameonya kuwa nchi yake itaridhia ushiriki wa kijeshi kwa wale watakaokiuka anga zake. Davutoglu amesema hata kama ni ndege atakayepita katika anga hizo atasimamishwa.

Ndege za kivita za Urusi zimekuwa zikiruka katika eneo la Syria tangu siku ya Jumatano wakishambulia kutoka angani kwa kila urusi inachokiita mashambulizi katika ngome za wanamgambo wa dola la kiislamu, pamoja na makundi mengine ya kigaidi katika maeneo ya Kaskazini na mikoa ya kati nchini Syria.

Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet Davutoglu
Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmet DavutogluPicha: Reuters/U. Bektas

Hata hivyo nchi za Magharibi zimesema Urusi inatumia nafasi hiyo kuwashambulia wapinzani wa Rais Bashar al Assad.

Uturuki na Urusi zimeendelea kuzozana katika mgogoro huu wa Syria, Moscow ikiwa mshirika wa Assad na Uturuki ikishikilia msimamo wake kuwa kuondoka kwa Assad ndiyo njia pekee ya kupata suluhu ya mgogoro wa Syria.

Jumuiya ya kujihami NATO yatoa onyo kwa Urusi

Kwa upande mwengine Jumuiya ya Kujihami ya Nato imeitolea wito Urusi kusitisha mara moja mashambulizi yake kwa raia wa Syria na upinzani na kuonya pia dhidi ya kukiuka anga za Uturuki. Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema vitendo kama hivyo vinaweza kusababisha hatari kubwa.

"Naitolea mwito Urusi kuepusha kueneza mvutano na muungano, Urusi inapaswa Kuepusha pia migongano ya kijeshi nchini Syria, pia nina wasiwasi kuwa Urusi haiwalengi wanamgambo wa IS na badala yake inawalenga upinzani na raia" alisema Jens Stoltenberg.

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg
Katibu Mkuu wa NATO Jens StoltenbergPicha: picture-alliance/dpa/J: Warnand

Wakati huohuo zaidi ya makundi 41 ya waasi nchini Syria yameapa kushambulia vikosi vya Urusi wakilipiza kisasi kutokana na mashambulizi ya angani yanayofanywa na nchini Syria.

Makundi hayo yamesema yataungana pamoja kama ishara ya Umoja, yamesema Urusi imejiingiza katika vita hivyo baada ya kuona vikosi vya rais Bashar al Assad vinaelekea kushindwa.

Mwandishi Amina Abubakar/Reuters/AFP/AP

Mhaririri : Mohammed Abdul-Rahman