Urusi yawahamisha raia wake kutoka eneo la Kursk
13 Agosti 2024Picha zilizochapishwa na Wizara ya dharura ya Urusi, zimewaonesha wakaazi wa eneo la mpaka la Kursk wakiwasili katika vituo vya makazi ya muda Moscow. Kwa ujumla, Urusi imelazimika kuwaondoa takriban raia 200,000 kwenye mkoa huo wiki moja baada ya wanajeshi wa Ukraine kuuvamia.
Soma zaidi: Putin: Mashambulizi ya Ukraine hayatazima oparesheni yetu
Ukraine kwa upande wake imesema haina nia ya kuitwaa sehemu hiyo ya Urusi baada ya kuidhibiti katika hatua ya kushtukiza ya wiki moja iliyopita. Kyiv imeongeza kuwa itaacha kufanya mashambulizi ya aina hiyo ikiwa Moscow itakubali amani kwa njia ya haki. Zaidi msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Ukraine amesisitiza kuwa hatua zilizochukuliwa na wanajeshi wa nchi hiyo dhidi ya Urusi ni halali.
Urusi yawazuia wanajeshi wa Ukraine kujipenyeza zaidi kwenye himaya yake
Hayo yanajiri wakati Wizara ya Ulinzi ya Urusi ikiarifu kuwa imefanikiwa kuyazuwia mashambulizi mapya ya wanajeshi wa Ukraine waliokuwa kwenye magari ya kivita wakiwa na makombora, na droni walipokuwa wakielekea ndani ya vijiji kadhaa vya Urusi.
Kauli ya wizara hiyo imesema Urusi ilitumia idara zake za jeshi, wanajeshi wapya wa ziada, ndege za kivita, droni na vikosi vya mizinga kuzuia wanajeshi wa Urusi wasijipenyeze zaidi ndani ya taifa hilo. Akilizungumzia hilo, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Ukraine Heorhii Tykhyi amesema operesheni hiyo ya nje ya mipaka yake ililenga kuilinda Kyiv dhidi ya mashambulizi ya Urusi .
Soma zaidi: Urusi na Ukraine zaendeleza mapambano
Katika tukio jingine, Raia wawili wa Urusi wameuwawa baada ya wanajeshi wa Ukraine kulilipua basi lililokuwa na raia katika mji wa Lysychansk wa Ukraine unaodhibitiwa na Urusi. Hayo ni kwa mujibu wa shirika la habari la nchini Urusi la TASS lililozinukuu mamlaka za Urusi. Maafisa wa mji huo, hapo awali walisema kuwa zaidi ya watu 30 wamejeruhiwa kutokana na shambulio hilo.