Urusi yavujisha nyaraka za siri za maafisa wa Ujerumani
3 Machi 2024Wanasiasa wa upinzani nchini Ujerumani wamependekeza Jumapili uchunguzi ufanyike bungeni, ikiwa ni pamoja na maswali kwa Kansela Olaf Scholz, baada ya Urusi kusambaza sauti ya maafisa wakuu wa jeshi wakijadili taarifa za siri kuhusu silaha za Ukraine.
Kamishna maalum wa bunge katika jeshi, Eva Högl kutoka chama cha Social Democrats cha Kansela Olaf Scholz, ametoa wito wa kuboreshwa kwa mafunzo kuhusu mawasiliano salama kwa maafisa wakuu wa kijeshi.
Haya yanajiri baada ya mkuu wa shirika la utangazaji la serikali ya Urusi RT, Margarita Simonyan, siku ya Ijumaa kuvujisha rekodi ya sauti ya zaidi ya dakika 30 ya maafisa wanne wa Ujerumani wakijadili uwezekano wa kutuma makombora ya Taurus kwenda Ukraine.
Wizara ya Ulinzi ya Ujerumani imesema inaamini kuwa sauti hiyo ilikuwa ya kweli na kwamba mazungumzo hayo yalinaswa kwa njia ya simu.
Mjadala wa uwezekano wa kutuma makombora ya Taurus kwenda Ukraine ulijadiliwa wiki hii, huku Scholz akisema haitawezekana kwa sababu ingehitaji wanajeshi wa Ujerumani kwenda nchini Ukraine au angalau kushirikiana moja kwa moja kwenye operesheni ya kijeshi.