1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yauteka mji wa kitovu cha shughuli za reli wa Lyman

27 Mei 2022

Vikosi vya Urusi mashariki mwa Ukraine vimechukua udhibiti wa mji wa kitovu cha shughuli za reli wa Lyman na kuuzingira mji mwengine wa Sievierodonetsk.

https://p.dw.com/p/4By1C
Ukraine Russland Konflikt | Donbass-Region
Picha: ARIS MESSINIS/AFP via Getty Images

Maafisa wa Ukraine wamekiri leo kwamba kwa mji wa Lyman umetekwa na vikosi vya Urusi, japo wamesisitiza kuwa wapiganaji wake wanaendelea na mapambano katika eneo la mashariki la Donbas licha ya mafanikio ya wazi ya vikosi vya Urusi katika miji miwili ya eneo hilo.

Makundi yanayotaka kujitenga na ambayo yanaungwa mkono na Moscow yamesema sasa yanaudhibiti kikamilifu mji wa Lyman, kitovu cha shughuli za usafirishaji kwa njia ya reli ambacho kimekuwa kikishambuliwa na Urusi kutoka upande wa kaskazini.

Soma pia: Ukraine: Zelensky awasihi wanajeshi wa Urusi wasipigane

Wizara ya ulinzi ya Ukraine hata hivyo imesema wanajeshi wake wanapambana kufa kupona kuvizuia vikosi vya Urusi kuingia katika wilaya za kaskazini mashariki na kusini magharibi hasa kuelekea mji wa Sloviansk, mji uliopo umbali wa nusu saa upande wa kusini magharibi mwa Ukraine.

Ama kuhusu eneo la mashariki, gavana wa jimbo la Luhansk Serhiy Gaidai amesema vikosi vya Urusi vimeuzingira karibu mji wote wa Sievierodonetsk. Mji huo bado uko chini ya udhibiti wa serikali ya Ukraine.

Naye Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesisitiza msimamo wake kwamba Ujerumani imejitolea kimasomaso kuisaidia Ukraine.

Katika hotuba aliyoitoa katika mkutano uliofanyika mji wa kusini magharibi wa Stuttgart, Scholz amesema, "Na ndio maana tunaiunga mkono Ukraine. Ukraine pia inapata uungwaji mkono kutoka kwa washirika wetu. Na tumekubaliana kutofanya chochote kuihusisha NATO na mzozo huu maana utakuwa mzozo kati ya mataifa yenye nyuklia. Ni suala la kumwambia wazi Putin kwamba hakutakuwa na mkataba wa amani wenye masharti. Ukraine haitokubali, na sisi pia hatutokubali."

UNHCR imesema wakimbizi milioni 6.6 wa Ukraine wameikimbia nchi hiyo

Polen  Przemysl | Notunterkunft für Ukraine-Flüchtlinge
Wakimbizi wa Ukraine wakijifadhi katika kituo cha muda cha PrzemyslPicha: Nicolas Economou/NurPhoto/picture alliance

Umoja wa Mataifa umesema leo kuwa, kati ya wakimbizi milioni 6.6 wa Ukraine walioikimbia vita hivyo, wakimbizi milioni 2.9 wametafuta hifadhi katika mataifa mengine ya Ulaya.

Soma zaidi: Urusi: Mamia ya askari wa Ukraine wamejisalimisha

Wakimbizi hao, ambao idadi kubwa ni wanawake na watoto, wamevuka mipaka na kuingia mataifa jirani tangu uvamizi wa Urusi mnamo Februari 24.

Takwimu hizo kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi la UNHCR, zinaonyesha taswira kamili ya idadi ya wakimbizi waliosalia katika nchi ya kwanza waliyoingia na wangapi walielekea katika mataifa mengine kufuatia vita hivyo ambavyo vimesababisha mzozo mkubwa wa kibinadamu duniani.

UNHCR kupitia msemaji wake Shabia Mantoo amesema idadi kubwa ya wakimbizi katika nchi zisizo jirani na Ukraine wameingia nchini Ujerumani, Jamhuri ya Czech na Italia. Kati ya wakimbizi milioni milioni 6.6, zaidi ya wakimbizi milioni 3.5 wameelekea nchini Poland.