Urusi yapinga ripoti inayolaumu Syria kwa shambulizi la gesi
8 Novemba 2017Urusi imepinga ripoti iliyowasilishwa mbele ya baraza la usalama la umoja wa mataifa inayoilaumu Syria kwa kutumia gesi ya sumu ya Sarin katika mashambulizi mjini Khan Sheikhun iliyosababisha vifo vya watu wengi wakiwemo watoto.
Naibu balozi wa Urusi Vladimir Safronkov amesema kazi ya jopo la uchunguzi ni wa kukatisha tamaa na akapendekeza kwamba jopo hilo linatumiwa na magharibi kutia doa serikali ya rais Bashar al-Assad.
Chombo cha uchunguzi wa pamoja (JIM) kilihitimisha katika ripoti hiyo mwezi uliopita kuwa, serikali ya Syria ilihusika na mashambulizi ya gesi ya sumu ya Sarin ya Aprili 4 katika eneo la Khan Sheikhun ambayo iliwaua watu wengi ikiwa ni pamoja na watoto.
Urusi, mshirika wa Syria, na Marekani wameweka miswada yao ya maazimio yenye kukinzana juu ya kurefusha shughuli za jopo hilo itakayokamilika mnamo Novemba 16.
"Tuna hakika kuwa utaratibu huo, ulio na jukumu la juu, hauwezi kufanya kazi kwa njia hii," Safronkov aliiambia baraza hilo. "Bila mabadiliko ya kina, itakuwa chombo cha kuvutana na serikali ya Syria", alisema.
Urusi inasisitiza kuwa ripoti hiyo haiaminiki kwa sababu wataalamu hawakuenda katika eneo lililoathirika la Khan Sheikhun na badala yake kuchunguza sampuli zisizo za kweli.
Akiwasilisha matokeo, Edmond Mulet, mkuu wa jopo hilo, amesema wataalamu wamegundua kuwa sumu ya gesi ya Sarin ilidondoshwa kutoka angani na kwamba ndege za Syria zilikuwa katika eneo hilo ambapo shambulio lilifanyika.
Uchambuzi wa gesi ya sarin iliotumiwa katika eneo la Khan Sheikhun ilifanana na gesi inayoathiri neva iliyopatikana katika hifadhi ya Syria, Mulet alisema, akiongezea kwamba utungaji huu utakuwa vigumu sana kuuiga.
Safronkov alijibu kwamba "kemikali zinaweza kuwa zinazozalishwa mahali popote kuathiri kwa makusudi serikali ya Syria."
Marekani tena ilitoa wito wa kuongezwa shughuli za jopo hilo lililoanzishwa mwaka 2015 ili kubaini mhusika wa mashambulizi ya kemikali ya vita vya miaka 6 ya Syria.
"Yoyote anayetuzuia sisi kufikia lengo hili anawasaidia na kuwahimiza wale ambao wamekuwa wakitumia silaha za kemikali nchini Syria”, alisema balozi wa Marekani Nikki Haley.
Ufaransa na Uingereza walijitokeza kuunga mkono matokeo hayo na walisema jopo hilo lazima liruhusiwe kuendelea na kazi yake wakati China, ambayo inafanya kazi kwa karibu na Urusi katika baraza, ikitoa wito wa makubaliano.
Rasimu ya azimio la Urusi imetoa wito wa kurefushwa kwa miezi sita shughuli ya jopo hilo lakini ilisema itahifadhi matokeo yake juu ya eneo la Khan Sheikhun hadi wakati uchunguzi kamili na wenye ubora wa eneo hilo utakapowezekana.
Urusi imesema inahitaji kuchunguza ripoti hiyo ya Khan Sheikhun kabla ya kuamua iwapo jopo hilo litaendelea na shughuli zake.
Hakujakuwa na ombi la kupiga kura katika baraza hilo kutoka Marekani au Urusi na wanadiplomasia wanasema majadiliano yanaendelea.
Balozi wa Italia Sebastiano Cardi aliwaambia waandishi habari baada ya mkutano kuwa kuna uungwaji mkono wa nguvu wa kufufua upya mamlaka ya Chombo cha uchunguzi wa pamoja, JIM na kwamba makubaliano yanawezekana.
Mwandishi: Fathiya Omar/AFPE
Mhariri: Josephat Charo