Uingereza yatishia hatua kali dhidi ya Urusi
14 Machi 2018Uhusiano kati ya Uingereza na Urusi umezorota kwa haraka katika kipindi cha siku kumi tangu jasusi wazamani Sergei Skripal na binti yake Yulia waliposhambuliwa kwa sumu mjini Salisbury kaskazini magharibi mwa Uingereza.
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May alisema hapo jana kuna uwezekano mkubwa kuwa Urusi inahusika kwa njia moja au nyingine na shambulizi hilo kwa sababu imeshindwa kudhibiti sumu hiyo na kutaka Urusi itoe majibu katika kipindi cha saa 24 ambazo zimemalizika usiku wakuamkia leo.
Msemaji wa ubalozi wa Urusi mjini London amesema Urusi haitatekeleza wito huo hadi pale itakapo pokea sampuli ya kemikali hiyo huku pia Urusi ikitoa mwito kufanyika uchunguzi wa pamoja kuhusiana na tukio hilo.
Msemaji wa ubalozi huo wa Urusi mjini London ameongeza kuwa Urusi haikuhusika na shambulizi hilo na kuongeza kuwa nchi yake itajibu hatua yoyote itakayochukuliwa kama adhabu dhidi yake kuhusiana na tuhuma hizo.
Bi Theresa May amesema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya Urusi iwapo itashindwa kutoa maelezo ya kina kuhusiana na tuhuma hizo kufikia usiku wa kuamkia leo Jumatano.
Hatua zinazofikiriwa ni pamoja na kuzuia mali za viongozi wa Urusi pamoja na maafisa wengine wa nchi hiyo , kuzuia Urusi kuwekeza katika masoko ya kifedha ya Uingereza pamoja na kuwafukuza wanadiplomasia wa nchi hiyo.
Waziri Mkuu Theresa May anatarajia kuainisha hatua hizo katika bunge leo Jumatano baada ya mkutano wa baraza la usalama la taifa.
Uingereza yaomba ushirikiano kwa washirika
Uingereza pia inaripotiwa kutoa mwito kwa washirika wake wa nchi za magharibi kwa ajili ya ushirikiano wa pamoja juu ya sakata hilo.
Hayo yanajiri huku Umoja wa Ulaya ukiahidi kuipa ushirikiano Uingereza katika mzozo huo na Urusi.
Ahadi hiyo iliyotolewa na makamu wa rais wa halmashauri ya Ulaya Valdis Dombrovskis ina kuja mnamo wakati kukiwa na wasiwasi nchini Uingereza kuhusu ushirikiano wa kiusalama baada ya nchi hiyo kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya mwishoni mwa Machi 2019.
Naye msemaji wa mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federeca Moghereni amelieleza shirika la habari la Reuters kuwa matumizi ya silaha za sumu katika jaribio la kuwaua raia nchini Uingereza ni suala linalostua hivyo Umoja wa Ulaya unaungana na Uingereza katika kuhakikisha haki inapatikana na kuahidi kutoa ushirikiano itakapolazimu.
Rais wa Marekani Donald Trump amemueleza waziri mkuu Theresa May kwa njia ya simu kuwa Urusi inapaswa kutoa majibu yasiyo kuwa na utata kuhusiana na jinsi gani silaha hii ya sumu iliyotengenezwa Urusi ilivyotumika nchini Uingereza hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa ikulu ya White House.
Akizungumza na waandishi wa habari Trump ameongeza kuwa pindi watakapo pata ukweli juu ya tuhuma hizo basi wataishutumu Urusi au yeyote anayehusika.
Kwa upande mwingine waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson alizungumza na mawaziri wenzake wa Ufaransa na Ujerumani pamoja na Katibu Mkuu wa NATO- Jens Stoltenberg na kusema iwapo itathibiitishwa Urusi kuhusika na tuhuma hizo basi huu utakuwa ni uzembe unaotishia Jumuiya ya kimataifa.
Mwandishi : Isaac Gamba/ AFPE
Mhariri : Daniel Gakuba