1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yasema mazungumzo ya amani na Ukraine yanaendelea

Sylvia Mwehozi
6 Aprili 2022

Msemaji wa Ikulu ya Urusi Kremlin, Dmitry Peskov amesema mazungumzo ya kusaka amani na Kyiv yanaendelea licha ya ripoti za uhalifu wa kivita dhidi ya raia katika mji wa Bucha.

https://p.dw.com/p/49YIq
Ukraine, Borodjanka | Anwohner sucht in den Wohnhaustrümmern nach Habseligkeiten
Picha: Vadim Ghirda/AP/dpa/picture alliance

Peskov amesema kwamba mazungumzo na Ukraine yanaendelea lakini ripoti za mauaji ya Bucha ambayo ameyataja kama "yakupangwa" yameathiri mazungumzo hayo na hivyo safari bado ni ndefu. Peskov amesisitiza kwamba wangependa kuona mabadiliko zaidi kutoka upande wa Ukraine. Tangu mazungumzo ya pande zote yaliyofanyika Uturuki, wajumbe wa Urusi na Ukraine wameendelea na majadiliano kwa njia ya video.Zelenskiy alihutubia Baraza la Usalama, ataka Urusi iwajibishwe

Ama kwa upande mwingine, madai ya uhalifu wa kivita mjini Bucha yameendelea kutawala mzozo huo kwa hivi sasa. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amelieleza bunge la Ujerumani siku ya Jumatano kwamba "askari wa urusi walitekeleza mauaji ya raia wa Ukraine kabla waondoe vikosi vyake".

"Picha za kutisha kutoka Bucha zilitushtua sote sana. Kabla ya kuondoka wanajeshi wa Urusi walifanya mauaji ya raia wa Ukraine wakiwemo watoto, wanawake na wazee. Madai ya kihuni yanayoenezwa na Urusi kwamba picha hizi ni za kupangwa yanawaangukia wale wanaoeneza uongo huu. Mauaji ya raia ni uhalifu wa kivita", alisema Scholz.

Deutschland | Olaf Scholz im Bundestag zu Waffenlieferungen an die Ukraine
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Markus Schreiber/AP Photo/picture alliance

Kuhusu suala hilo China imesema kwamba picha za miili ya raia waliouwawa ni "za kuogofya" lakini hakuna mtu anayepaswa kunyooshewa kidole cha lawama hadi pale ukweli utakapojulikana. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Zhao Lijian amewaeleza waandishi wa habari kwamba Beijing inaunga mkono jitihada na hatua zote "zinazofaa kupunguza mzozo wa kibinadamu'' nchini humo na iko "tayari kuendelea kufanya kazi pamoja na jumuiya ya kimataifa kuzuia madhara yoyote kwa raia.''

Mazungumzo yamekwama baina ya Ukraine na Urusi

Naye waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban ambaye alichaguliwa tena kwa muhula mwingine siku ya Jumapili amemtaka rais Vladimir Putin wa Urusi kukubali usitishaji mapigano mara moja nchini Ukraine na kuwaalika viongozi wa Ufaransa, Ujerumani na Ukraine kukutana na kiongozi wa Urusi mjini Budapest.

Hungary pia imedokeza utayari wake wa kulipa gesi ya Urusi kwa sarafu ya Ruble na hivyo kutofautiana na Umoja wa Ulaya ambao umejaribu kuwa na msimamo mmoja wa kupinga masharti ya Moscow yanayotaka malipo kufanyika kwa sarafu ya nchi hiyo. 

Wakati huohuo Marekani, Umoja wa Ulaya na kundi la nchi zenye uchumi mkubwa duniani G7 zinatarajiwa muda wowote kutangaza vikwazo vikali dhidi ya Urusi. Vikwazo hivyo vinaweza kujumuisha marufuku ya uwekezaji sambamba na uagizaji mafuta na gesi kutoka Urusi.

Na mkuu wa jumuiya ya kujihami NATO Jens Stoltenberg amesema hakuna dalili kwamba Rais wa Urusi Vladimir Putin ana dhamira ya kuacha "kudhibiti Ukraine nzima" na vita hivyo vinaweza kudumu kwa muda mrefu.

Vyanzo: ap/reuters/afp/dpa