1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yasema haitaki vita na Uturuki

30 Novemba 2015

Waziri wa Uturuki anayeshughulikia uhusiano na Umoja wa Ulaya amesema nchi yake haiwezi kuwa na uhusiano wa kiadui na Urusi, baada ya ndege ya kijeshi ya Urusi kutunguliwa na Uturuki.

https://p.dw.com/p/1HCqy
Waziri wa Uturuki anayeshughulikia masuala ya Ulaya, Volkan BozkirDer türkische Europaminister Volkan Bozkir
Waziri wa Uturuki anayeshughulikia masuala ya Umoja wa Ulaya, Volkan BozkirPicha: DW/Ö. Coskun

Waziri wa Uturuki anaeshughulikia masuala ya Umoja wa Ulaya Volkan Bozkir amesema mjini Ankara kwamba anatumai nchi yake itaendeleza uhusiano na Urusi hata baada ya kutokea kadhia ya kutunguliwa ndege ya Urusi na walinzi wa Uturuki.

Uturuki imesema ndege hiyo iliingia katika anga ya Uturuki kwa sekunde kadhaa na imethibitisha kauli hiyo kwa kutoa ukanda ulionakili mawasiliano baina ya walinzi wa Uturuki na rubani wa ndege ya Urusi. Uturuki imesema rubani huyo alipewa onyo. Ukanda huo uliokabidhiwa kwa shirika la habari la AP unathibitisha kwamba rubani wa ndege ya Urusi alionywa mara kadhaa.

Lakini Urusi imekanusha taarifa hiyo. Rubani wa Urusi alienusurika amesema ndege yake haikuingia katika anga ya Uturuki na pia amekanusha madai kwamba alionywa mara kadhaa.

Hata hivyo Waziri wa mambo wa nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema licha ya kadhia hiyo Urusi haitaingia vitani na Uturuki. Lavrov amesema nchi yake haitapigana vita na Uturuki. Lakini amesema Urusi inayo maswali ya kuiuliza serikali ya Uturuki. "Tuna mashaka iwapo mkasa huo ulitokea kwa bahati mbaya. Inaonekana kana kwamba kadhia hiyo ni uchokozi uliopangwa."

Waziri wa mambo wa nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema nchi yake itatathmini upya makubaliano yote iliyofikia na Uturuki. Hata hivyo waziri Lavrov amesema watu wa Urusi hawaubadili mtazamo wao juu ya Waturuki. Wakati huo huo, Urusi imeimarisha ukaguzi wa bidhaa za chakula na kilimo kutoka Uturuki. Wizara ya kilimo imesema imeiarifu mamlaka inayoshughulikia usalama wa chakula kuimarisha ukaguzi. Hatua hiyo imechukuliwa baada ya utafiti wa wizara kubainisha kwamba bidhaa za kilimo zinazoingia nchini kutoka Uturuki hazitimizi viwango.

Mwandishi: Abdu Mtullya

Mhariri: Daniel Gakuba