Urusi yasalimu amri mbele ya Uruguay
25 Juni 2018Urusi ambayo ilianza vizuri mashindano haya ya kombe la dunia wakiwa wenyeji wa mashindano haya, walishindwa kuhimili vishindo vya Uruguay kutoka Amerika ya kusini kwa kukubali kipigo cha mabao 3-0 na kuridhika na nafasi ya pili kutoka katika kundi A. Urusi , ambayo imekwisha fuzu kucheza katika duru ya timu 16 za mtoano pamoja na Uruguay , baada ya kushinda michezo yake miwili ya mwanzo ilicheza muda mwingi wa mchezo huo wakiwa na watu 10 uwanjani baada ya Igor Smolnikov kutolewa kwa kadi ya pili ya njano baada ya dakika 36. mabao ya Luis Suarez, bao la la kujifunga wenyewe la Denis Cheryshev na bao la dakika za mwisho la Edinson Cavani yaliwahakikishia Uruguay ushindi wa kwanza katika kundi hilo A.
Suarez alifungua kitabu cha mabao kwa Uruguay katika dakika ya 10 ya mchezo akifunga bao lake la saba katika kombe la dunia na ushindi wa Uruguay uliongezeka pale Diego Laxalt alipopiga shuti katika dakika ya 23 na kumgonga Cheryshev na kujaa wavuni.
Na mjini Volgograd , saudi Arabia iliishinda Misri kwa mabao 2-1 katika mchezo ambao ulikuwa ni wa kutimiza wajibu. Salman Al-Faraj alipiga mkwaju wa penalti kwa upande wa Saudi Arabia katika mchezo mwingine wa kundi A dhidi ya Misri, na ulikuwa mchezo wa 18 wa kombe la dunia na ulikuwa sawa na idadi ya mashindano ya kombe la dunia mwaka 2002 yaliyofanyika Japan na Korea kusini. Katika mashindano yaliyofanyika nchini Brazil miaka minne iliyopita , kulikuwa na mikwaju 13 ya penalti katika mashindano yote.
Matumizi ya vidio kuwasaidia waamuzi VAR yamechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la penalti, na mfumo huo ulitumika tena kumzawadia Al-faraj mkwaju wa penalti. Penalti hiyo iliyopigwa na Al-Faraj ni ya pili katika mchezo huo.
Fahad Al-Muwallad alipewa mkwaju wa penalti baada ya kuchezewa vibaya ndani ya box katika dakika ya 39 lakini juhudi zake hazikuzaa matunda.
Kwa upande wa Misri , Mohamed Salah alipachika bao katika dakika ya 22 na Salman Al-Faraj alisawazisha bao hilo kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika. Baada ya hapo Saudi Arabia walifanikiwa kupata ushindi muhimu na kumaliza kundi hilo wakiwa katika nafasi ya tatu , ba ada ya salem Al-Dawsari kufunga bao katika dakika ya 95.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Bruce Amani