1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yapongeza hatua ya Syria

13 Septemba 2013

Rais wa Urusi, Vladmir Putin amesema hatua ya Syria kujiunga na mkataba wa kimataifa wa kudhibiti matumizi ya silaha za sumu, imedhihirisha imani yake njema na inatoa onyo kali kwa Marekani kutoivamia kijeshi nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/19h2i
Rais wa Urusi, Vladimir Putin
Rais wa Urusi, Vladimir PutinPicha: picture-alliance/dpa

Akizungumza katika mkutano muhimu wa Umoja wa Mataifa kuhusu jinsi jumuiya ya kimataifa inavyoweza kudhibiti silaha za kemikali, mjini Geneva, Uswisi, Rais Putin amesema kuwa ana matumaini kwamba hatua hiyo itafungua hatua muhimu kuelekea katika kuutatua mzozo wa Syria.

Jana Alhamisi, Syria ilifanya jitihada rasmi za kujiunga na mkataba wa kimataifa wa kudhibiti matumizi ya silaha za sumu, hatua ambayo imepongezwa pia na Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, umoja huo umesema kuwa itachukua takribani siku thelathini kwa Syria kuwa mwanachama wa mkataba huo.

Pendekezo hilo lilitolewa na Urusi

Jumatatu iliyopita, Urusi ilipendekeza Syria ijiunge na mkataba huo ili kuepuka kuvamiwa kijeshi na Marekani. Aidha, wanadiplomasia kadhaa wa Umoja wa Mataifa wamesema hawana uhakika iwapo Syria imetekeleza masharti yote ili kujiunga rasmi katika mkataba huo.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry na mwenzake wa Urusi, Sergei LavrovPicha: Reuters

Ama kwa upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry na mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, leo wamekutana na Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Lakhdar Brahimi, katika juhudi za kuzuia hatua yoyote ya kijeshi inayoweza kuchukuliwa na Marekani.

Viongozi hao wamesema wana matumaini kwamba mazungumzo kuhusu silaha za kemikali za Syria, yatasaidia kufufua mpango wa kimataifa wa kufanyika mazungumzo ya awamu ya pili mjini Geneva yenye lengo la kutafuta njia ya kumaliza vita vya Syria.

Mazungumzo hayo ya Geneva, ni sehemu ya juhudi za kidiplomasia zilizomshawishi Rais Barack Obama wa Marekani kusitisha mpango wake wa kuishambulia Syria kijeshi, katika kujibu shambulio la silaha za kemikali dhidi ya raia lililofanywa katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi, Agosti 21, mwaka huu. Jana Alhamisi, Kerry alisema kuwa Marekani inaweza kuishambulia Syria kijeshi, iwapo haitaridhika kwa sababu hilo siyo suala la mchezo.

Marekani na washirika wake wamlaumu Assad

Marekani na washirika wake wanasema kuwa majeshi ya Rais Bashar al-Assad yalifanya shambulio la gesi ya sumu ya Sarin na kuwaua zaidi ya watu 1,400. Hata hivyo, Putin na Assad, wanavilaumu vikosi vya waasi kwa kuhusika na shambulio hilo.

Baada ya mkutano wa leo, Kerry, amesema atakutana tena na Lavrov mjini New York baadae mwezi huu wa Septemba, ili kupanga tarehe ya mkutano wa amani kwa ajili ya Syria, uliosubiriwa kwa muda mrefu.

Rais wa China, Xi Jinping
Rais wa China, Xi JinpingPicha: Getty Images/Ria Novosti/Igor Russak

Rais wa China, Xi Jinping, amesema kuwa nchi yake inaunga mkono juhudi za Urusi na iko tayari kusaidia juhudi za kisiasa kuhusu mzozo wa Syria katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kwa upande wake rais wa Iran, Hassan Rouhani, amesema pia anaunga mkono mpango wa Urusi na kwamba nchi yake iko tayari kusaidia mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Assad na upinzani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,APE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman