Urusi yapambana na moto karibu na kituo cha nyuklia
12 Agosti 2010Serikali ya Urusi imepeleka treni maalum ya kuzima moto na watu wengine 70 kuwasaidia zaidi ya wazima moto 3,400 wanaopambana na moto kwenye misitu iliyo karibu na kituo kikuu cha utafiti wa nyuklia. Moto haujafika kwenye eneo la kituo hicho cha nyuklia cha Sarov,lakini hifadhi ya misitu iliyo karibu,imeshika moto tangu kiasi ya juma moja lililopita. Kama watu 50,000 wanapambana na moto katika eneo hilo katikati ya Urusi.
Kwa mujibu wa msemaji wa wizara ya huduma za dharura, Mikhail Turkov, ndege mbili na helikopta mbili zinazunguka eneo la Sarov kuchunguza mkondo wa moto. Amesema, wanajeshi wawili waliuawa walipokuwa wakizuia moto huo kukaribia kituo cha nyuklia cha Sarov. Msemaji wa kituo hicho amelithibitishia shirika la habari la AFP kuwa moto haujafika kwenye kituo hicho na wafanyakazi wake wala hawakuhamishwa, lakini hakutaka kutoa maelezo zaidi.
Hata hivyo kuna wasiwasi mkubwa kuhusu misitu iliyoshika moto ambayo ilichafuliwa na chembe chembe za nyuklia katika mwaka 1986 kufuatia ajali iliyotokea kwenye mtambo wa nyuklia wa Chernobyl.
Vladimir Stepanov alie mkuu wa kituo kinachoshughulikia masuala ya dharura, anasema, viwango vya miale ya sumu ya nyuklia havikupindukia kiwango cha kawaida. Serikali ya Urusi inajaribu kutuliza hofu kuwa moto huo wa misituni huenda ukatimua chembe chembe za nyuklia zilizoko ardhini. Lakini muasisi wa shirika linalotetea mazingira "Greenpeace" nchini Urusi, Alexei Yablokov anasema, chembe chembe za nyuklia zinaweza kutawanyika umbali wa mamia ya kilomita kwa kutegemea hali ya hewa.
Wataalamu wanasema Urusi inakabiliana na wimbi la joto kali kabisa katika historia yake. Moto huo umeathiri kila sekta ya maisha na inatathminiwa kuwa pato la jumla la ndani huenda likapunguka kwa asilimia moja.
Mwandishi:P.Martin/AFPE
Mhariri:M.Abdul-Rahman