1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaishambulia Ukraine kwa kombora la kuvuka mabara

21 Novemba 2024

Baada ya Ukraine kuishambulia Urusi kwa makombora ya Marekani na Uingereza, Urusi kwa mara ya kwanza yatumia kombora la kuvuka mabara kuishambulia Ukraine.

https://p.dw.com/p/4nEl2
Makombora ya atomiki aina ya Topol-M
Wanajeshi wa Urusi wakiwa na makombora ya kuvuka mabara aina ya Topol-MPicha: ARTYOM KOROTAYEV/AP/picture alliance

Urusi imefyetuwa kombora la kuvuka mabara leo (Alhamisi) asubuhi kutokea mkoa wake wa kusini wa Astrakhan  kuishambulia Ukraine, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kwa nchi hiyo kutumia silaha zenye nguvu kubwa namna hiyo tangu ilipoanzisha vita hivyo.

Jeshi la anga la Ukraine ambalo limetowa ripoti hiyo limesema kwamba shambulio hilo la Urusi limeilenga miundo mbinu kadhaa muhimu katika mji wa Dnipro.

Shambulio hilo la Urusi linashuhudiwa ikiwa ni baada ya Ukraine nayo siku ya Jumanne kwa mara ya kwanza kutumia makombora yaliyotoka Marekani na Uingereza kuishambulia Urusi, hatua ambayo Urusi ilishatowa tahadhari miezi kadhaa nyuma,  kuionya Ukraine kwamba itazidisha makali kwenye vita hivyo.

Mazoezi makubwa ya kijeshi ya NATO- Finnland
Nato ikifanya mazoezi makubwa ya kijeshi FinnlandPicha: DW

Haijakuwa wazi kutoka Ukraine juu ya uharibifu uliofanywa na shambulio hilo la leo la Urusi la kombora la masafa marefu.Soma pia: Korea Kaskazini yarusha kombora la ICBM wakati Marekani, Seoul zikiisokoa kutuma jeshi Urusi

Lakini pia Urusi kupitia msemaji wake wa wizara ya mambo ya nje Maria Zakharova, imesema iko tayari kutafakari juhudi zozote za kweli za kuleta amani  katika mgogoro huo na ambazo zitazingatia maslahi yake na hali halisi ya vita hivyo, lakini sio juhudi zenye mirengo ya kisiasa.

Marekani Jumatano  ilitangaza inataka kuipelekea Ukraine mabomu ya kutega ardhini ili kuisaidia nchi hiyo kuvirudisha nyuma vikosi vya Urusi.

Hatua hiyo imekosolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Human rights Watch kutokana na athari zinazoweza kusababishwa na mabomu hayo kwa raia .

Rais Volodymyr Zelensky amefurahishwa na uamuzi huo wa Marekani akisema mabomu hayo ni muhimu sana katika kuyazuia mashambulizi ya Urusi.

Kombora la masafa marefu la kuvuka mabara
Kombora la kuvuka mabaraPicha: Jim Lo Scalzo/dpa/picture alliance

Kufuatia hali inayoendelea hivi sasa kwenye vita hivyo, Hungary imesema itaweka mfumo wa ulinzi wa anga katika eneo lake la Kaskazini Mashariki kutokana na kitisho cha kutanuka kwa vita hivyo kuongezeka kwa namna ambayo haijawahi kutokea.

Jana Jumatano waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Kristof Szalay- Bobrovniczky  alisema bado wanaamini amani inaweza kupatikana hivi karibuni kupitia mchakato wa kidiplomasia na sio wa kijeshi lakini pia akasisitiza ni bora zaidi kujiandaa kwa lolote linaloweza kutokea.Soma pia: Vikosi vya Urusi vyadai kusonga mbele upande wa mashariki mwa Ukraine

Wasiwasi wa Hungary waongezeka

Uamuzi huo wa Hungary umefanyika baada ya mkutano wa baraza la ulinzi la nchi hiyo uliotishwa na waziri mkuu Viktor Orban kujadili kinachoendelea sasa katika vita vya Ukraine.

Viktor Orban na Zelensky wakiwa Kiev Ukraine
Viktor Orban na Zelensky wakiwa walipokutana KievPicha: Maxym Marusenko/Nur Photo/IMAGO

Itakumbukwa kwamba Hungary ni mshirika wa jumuiya ya kujihami ya NATO na pia mwanachama wa Umoja wa Ulaya lakini inagawana mpaka na Ukraine.

Jeshi la nchi hiyo hivi sasa liko kwenye mpango wa kuimarisha uwezo wake huku ikielezwa kwamba baadhi ya vikosi vyake vimeshawekwa katika hali ya tahadhari.

Kwa upande mwingine huko Laos mawaziri wa ulinzi wa mataifa ya Jumuiya ya kanda ya Kusini Mashariki mwa Asia-ASEAN wamekutana leo na naibu waziri wa ulinzi wa Korea Kusini Kim Seon ho amewaambia waandishi habari kwamba kupelekwa kwa vikosi vya Korea Kaskazini nchini Urusi ni kitendo cha uhalifu dhidi ya ubinadamu.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW