Urusi yadai Ukraine ilijaribu kuishambulia Kremlin
3 Mei 2023Video hiyo inaonyesha kifaa kinachoruka kikirabia kuba ya jengo la baraza la Seneti katika Kremlin, na kulipuka kabla ya kulifikia. Urusi imeituhumu Ukraine kuishambulia Kremlin kwa droni usiku wa kuamkia Jumatano, katika jaribio lililofeli la kumuuwa Rais Vladmiri Putin, shutuma ambazo Kyiv imekana.
Rais Putin hakuwepo Kremlin wakati shambulio hilo likitokea, ambapo msemaji wake Dmitry Peskov ameliambia shirika la habari la serikali ya Urusi Ria Novosti, kwamba rais huyo alikuwa katika makazi yake ya Novo-Ogaryovo, nje ya Moscow.
Hata hviyo hakukuwa na uhakiki huru wa shambulio hilo ambalo maafisa wa Urusi wanasema lilitokea usiku lakini bila kuwasilisha ushashidi kuthibitisha madai hayo. Na wala maafisa hao hawakusema kwanini imechukuwa zaidi ya masaa 12 kuripoti tukio hilo.
Soma pia: Ukraine yajiandaa kulipiza kisasi kwa kuishambulia Urusi
Mshauri wa rais wa Ukraine Mykhailo Podolyask amekanusha ushiriki wowote katika tukio hilo linalodaiwa kuwa ni shutuma kubwa zaidi ambayo Urusi imetoa dhidi ya Ukraine tangu kutuma wanajeshi kuivamia nchi hiyo jirani zaidi ya miezi 14 iliyopita.
"Ukraine haina uhusiano wowote na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwenye Kremlin," alisema. Alisema madai hayo yatatoa kisingizio kwa Urusi "kuhalalisha mashambulizi makubwa katika miji ya Ukraine, dhidi ya raia, na miundombinu" katika siku zijazo.
Ikulu ya Kremlin imesema ndege mbili zisizo na rubani zilitumika katika shambulio hilo linalodaiwa kuyalenga makazi ya Putin katika ngome ya Kremlin, lakini zilizimwa na mifumo ya ulinzi ya kielektroniki.
Imeongeza kuwa Urusi ina haki ya kulipiza kisasi, matamshini yanayoasharia kuwa Moscow inaweza kutumia tukio hilo kuhalalisha uzidishaji wa "operesheni yake maalum ya kijeshi" na Ukraine.
Shambulio hilo lililodaiwa lilisababisha miito nchini Urusi kutoka kwa watu wanaoiunga mkono Kremlin kufanya mauaji dhidi ya viongozi wakuu nchini Ukraine.
Zelenskiy: Putin anahaha kwa kukosa ushindi
Madai hayo yamekuja wakati Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy akifanya ziara isiyotangazwa mjini Helsinki kwa mazungumzo na viongozi wa nchi tano za Nordic, ambapo anajaribu kupata silaha zaidi zenye nguvu kwa ajili vikosi vyake vya jeshi wakati wanafikiria jinsi ya kuwaondoa wanajeshi wa Urusi kutoka maeneo yanayokaliwa ya Ukraine.
Zelenskiy aliuambia mkutano wa waandishi habari mjini Helsinki kabla ya shambulizi hilo la droni kwamba mashambulizi ya Ukraine yako karibuni sana, na kuongeza kuwa mwaka huu utakuwa wa maamuzi na ushindi.
Soma pia: Zelensky atoa wito wa Ukraine kupatiwa mifumo ya kisasa ya ulinzi wa anga
Lakini alivyolizungumzia alisema Ukraine haimlengi Putin. "Hatumshambulii Putin, au Moscow, tunapigana kwenye ardhi yetu."
Kremlin imedai kuwa shambulio hilo lilipangwa kuvuruga Siku ya Ushindi, ambayo inafanyika katika uwanja Mwekundu mnamo Mei 9 kuadhimisha ushindi dhidi ya Ujerumani ya Wanazi katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia, ambayo inatazamiwa kuhudhuriwa pia na viongozi wa kigeni.
Urusi yaendeleza mashambulizi Ukraine
Kwingineko, Urusi ilitumia ndege zisizo na rubani zilizotengenezwa na Iran katika shambulio lake la tatu kwenye mji mkuu wa Ukraine Kyiv, katika muda wa siku sita.
Milipuko ilisikika mjini Kyiv na kwingineko majira ya usiku wakati vmifumo ya ulinzi wa anga ya Ukraine ikidungua droni 21 za Urusi, imesema kamandi ya Jeshi la anga la Ukraine. Hakuna uharibifu au hasara iliyoripotiwa.
Wakati huo huo, moto mkubwa umezuka katika ghala la mafuta la Urusi, maafisa wa eneo hilo wamesema Jumatano.
Bohari hiyo ililipuka moto katika eneo la kusini mwa Urusi la Krasnodar, lililoko mashariki mwa Rasi ya Crimea inayoshikiliwa na Urusi, kulingana na Gavana wa Krasnodar Veniamin Kondratyev.
Chanzo: Mashirika