Urusi yadai kukiteka kijiji karibu na Bakhmut
9 Januari 2023Taarifa iliyotolewa Jumatatu na vikosi hivyo katika mtandao wa kijamii wa Telegram, imeeleza kuwa kijiji cha Bakhmutske katika eneo la Jamhuri ya Watu wa Donetsk kimekombolewa na Vikosi vya Wanajeshi wa Shirikisho la Urusi.
Kijiji hicho kiko kaskazini mashariki mwa Bakhmut, mji ambao Urusi imekuwa ikijaribu kuuteka kwa miezi kadhaa sasa. Kabla ya Urusi kuivamia Ukraine kilikuwa na wakaazi 70,000 na sasa kimegeuka kuwa eneo la mapambano. Kijiji hicho kiko nje kidogo ya mji wa Soledar ambao pia ni eneo la mapigano makali.
Bakhmut na Soledar maeneo ya mapambano makali
Katika hotuba yake ya Jumapili usiku, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema kwamba eneo kati ya miji ya Bakhmut na Soledar ni moja ya maeneo yenye umwagaji mkubwa zaidi wa damu katika mapambano. ''Hali katika maeneo ya mapambano haijabadilika sana katika wiki ya kwanza ya mwaka. Mapigano makali yanaendelea kwenye majimbo ya Luhansk na Donetsk. Leo kamanda wa vikosi, Jenerali Syrskyi amewatembelea wanajeshi wanaolinda viunga vya mji wa Bakhmut na Soledar,'' alifafanua Zelensky.
Mwezi Septemba, Urusi ilidai kujinyakulia Donetsk na majimbo mengine matatu ya Ukraine, baada ya kufanyika ''kura ya maoni'' isiyo halali ambayo haijatambuliwa na Ukraine na mataifa ya Magharibi.
Ama kwa upande mwingine, maafisa wa Ukraine wamesema Jumatatu kuwa vikosi vya Ukraine vimezuia mashambulizi ya mara kwa mara ya Urusi katika mji wa Bakhmut na miji mingine kwenye jimbo la mashariki la Donbas. Ukraine imekanusha madai ya Urusi kwamba wanajeshi 600 wameuawa katika shambulizi la kombora.
Jeshi la Urusi lilidai kufanya mashambulizi ya anga katika kambi ya kijeshi inayotumiwa na wanajeshi wa Ukraine ikiwa ni katika kilipa kisasi kutokana na vifo vya wanajeshi wa Urusi waliouawa kwenye shambulizi la roketi wiki iliyopiota.
Ripoti ya kila siku inayotolewa na jeshi ya Ukraine imeeleza kuwa Urusi siku ya Jumapili ilifyatua makombora saba, ilifanya mashambulizi 31 ya anga na mashambulizi 73 yaliyofyatuliwa na mtambo wa kurushia roketi aina ya Salvo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya jeshi, vikosi vya Ukraine vilizuia mashambulizi katika maeneo 14 yenye makaazi ikiwemo Bakhmut.
Vikosi vya Ukraine zinazuia Urusi kusonga mbele
Zelensky amesema ingawa eneo kubwa la mji wa Bakhmut limeharibiwa kwa mashambulizi ya Urusi, wanajeshi wa Ukraine wanaendelea kuzuia jaribio la Urusi kusonga mbele.
Aidha, Gavana wa Kharkiv, Oleh Synehubov amesema mwanamke mwenye umri wa miaka 60 ameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa katika shambulizi la kombora la Urusi lililotokea mapema Jumattau kwenye soko moja katika kijiji cha Schevchenkove, mashariki mwa Ukraine.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya OSCE, Helga Maria Schmid, amesema anaunga mkono Urusi kuendelea kuwa mwanachama wa shirika hilo, baada ya kuwepo wito wa kuitaka Urusi kufukuzwa kwenye kundi hilo lenye nchi wanachama 57 kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine.
(AFP, DPA, Reuters)