1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi, Ukraine zakubaliana na mpango wa amani wa Afrika

17 Mei 2023

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amesema marais wa Urusi na Ukraine wamekubali kuutafakari mpango wa amani wa nchi za Afrika juu ya kuvimaliza vita vya Ukraine.

https://p.dw.com/p/4RUHu
BRICS Treffen in Brasilien/Vladimir Putin und Cyril Ramaphosa
Picha: Mikhail Metzel/ITAR-TASS/IMAGO

Rais Ramaphosa amesema ujumbe wa viongozi wa nchi za Afrika utaenda Urusi na Ukraine kwa lengo la kusaidia kuvimaliza vita hivyo.

Ramaphosa aliyezungumza kwa njia ya simu na marais Vladimir Putin wa Urusi na Volodoymyr Zelensky wa Ukraine kwa nyakati tofauti amesema marais hao wamekubali kuwapokea wajumbe wa Afrika kwenye miji yao, ya Moscow na Kiev ili kuujadili mpango wa kuutatua mgogoro.

Ujumbe wa Afrika utazijumuisha, Senegal, Uganda, Misri, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Afrika Kusini.

Juhudi za nchi hizo za Afrika zinaungwa mkono na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na Umoja wa Afrika.