Urusi, Iran na Uturuki kupambana na ugaidi
20 Desemba 2016Urusi imeyasema hayo leo (20.12.2016) katika mkutano wa pamoja kati ya nchi hizo. Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Ravrov na mwenzake wa Uturuki Mevlut Cavusoglu wamefanya mikutano kadhaa mjini Moscow katika muendelezo wa mazungumzo yanayotazamiwa kujikita zaidi katika vita dhidi ya ugaidi.
Nchi zote mbili zimelaani shambulio la mauaji dhidi ya Balozi Andrey Karlov ambalo lilifanyika jana Jumatatu jioni, na kusema kuwa mauaji hayo ni uchochezi na yanalenga kuvuruga uhusiano baina ya nchi hizo. Na kisha kuongeza kuwa Urusi na Uturuki zitashirikiana katika kufanya uchunguzi wa tukio hilo ambapo mpaka sasa Moscow imeshatuma wataalam 18.
Msemaji wa Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema kuwa mauaji ya balozi huyo yanawafurahisha wale ambao wanataka kudhoofisha mazungumzo ya amani ya Syria.
Wakati hayo yakiriji, shirika la misaada ya kiutu la Umoja wa Mataifa limesema kuwa serikali ya Syria imeidhinisha mipango ya Umoja wa Mataifa ya kutuma maafisa karibu 20 kwa ajili ya kufuatilia zoezi la kuondoa raia kutoka katika baadhi ya maeneo ambayo yanashikiliwa na waasi mashariki mwa Aleppo.
Mipango hiyo inakuja baada ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kukubaliana kupitisha azimio siku ya Jumatatu la kutuma haraka wafuatiliaji.
Msemaji wa ofisi ya uratibu wa masuala ya kiutu Jens Laerk amesema kuwa maafisa hao wa Umoja wa Mataifa wataenda mapema kadri itakavyowezekana.
Mazungumzo kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa Urusi, Iran na Uturuki yalipangwa kufanyika leo hata kabla ya tukio la kuuwawa wa balozi wa Urusi nchi Uturuki lililotokea jana jioni mjini Ankara.
Mwandishi: Celina Mwakabwale/Reuters/DPA/AP
Mhariri:Iddi Ssessanga