Urusi yatuhumiwa kutaka kumuua mkuu wa kampuni ya Ujerumani
12 Julai 2024Wanasiasa wa Ujerumani wameghadhabishwa na baada ya ripoti moja ya shirika la habari la Marekani CNN kufichua madai kwamba Urusi ilikuwa inapanga kumuua mkuu wa kampuni ya Ujerumani ya utengenezaji silaha ya Rheinmetall. Kampuni hii ni muhimu kwa silaha ambazo Ujerumani inazipeleka Ukraine. Kulingana na ripoti hiyo iliyochapishwa jana, maafisa wa ujasusi wa Marekani wamefichua mipango ya serikali ya Urusi ya kumuangamiza Armin Papperger, afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Rheinmetall mapema mwaka huu.
Soma: SIPRI: Mapato ya makampuni makubwa ya silaha yapungua
Shirika la habari la CNN linasema maafisa wa Ujerumani walifahamishwa kuhusiana na njama hiyo na wakamuongezea ulinzi Papperger wakati huo. Kampuni ya Rheinmetall haijatoa tamko kuhusiana na ripoti hiyo. Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi katika bunge la Ujerumani, Bundestag, Marcus Faber, amesema hii inaonesha kwa mara nyengine kwamba Urusi inavisogeza vita vyake Ulaya.