Von der Leyen ataka muungano wa afya Ulaya
16 Septemba 2020Katika hotuba yake ya kwanza ya mwaka kuhusu hali ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen amesema janga la virusi vya corona limetilia mkazo haja ya ushirikiano wa karibu zaidi, akisisitiza kwamba watu wanaendelea kuteseka.
"Kwangu ni dhahiri shahiri: tunahitaji muungano imara wa afya wa Ulaya. Ni wakati wa kufanya hilo," amesema von der Leyen mbele ya bunge la Ulaya.
Amesema tume yake itajaribu kuuimarisha wakala wa dawa wa Ulaya na kituo cha kuzuwia na kudhibiti magonjwa. Na ametangaza pia kuundwa kwa wakala mpya wa utafiti wa dawa za kibayolojia na maendeleo, BARDA.
Soma pia: Mshikamano wa Ulaya watakiwa kupambana na Virusi vya Corona
Amesema atashirikiana na Italia wakati itakapochukua nafasi ya urais wa kupokezana wa kundi la mataifa 20 yaliostawi zaidi duniani, G20, kuitisha mkutano wa kilele wa afya wa viongozi wa dunia mwakani, ili kushirikishana mafunzo ya mzozo wa virusi vya corona.
Sera ya afya inasalia kuwa wajibu wa mataifa wanachama, na wakati Brussels imejaribu kuratibu uitikiaji wa kanda hiyo juu ya janga la corona, vizuizi vya kitaifa na sheria za mipakani vimetofautiana pakubwa.
Rais huyo wa halmashauri kuu ya Ulaya, ambae kitaaluma ni daktari, ameyaonya mataifa kutochukuwa hatua kwa ubinafsi litakapokuja suala la chanjo, ambayo inatazamwa na wengi kama suluhuhisho la kukomesha mzozo wa janga la corona.
Soma pia: Umoja wa Ulaya wakusanya fedha kukabiliana na COVID-19
Kupunguza utoaji gesi chafu kwa asilimia 55 kufikia 2030
Kuhusu suala la uhifadhi wa mazingira na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya amependekeza kupunguza utoaji wa gesi chafu barani Ulaya kwa asilimia 55 kufikia mwaka 2030, katika kuitikia dharura ya tabianchi.
"Natambua ongezeko hili kutoka asilimia 40 hadi 55 ni kubwa mno kwa baadhi, na siyo la kutosha kwa wengine. Lakini thathimini yetu ya athari inaonyesha wazi kwamba sekta zetu za uchumi wetu na viwanda zinaweza kumudu hili," amesema von der Leyen.
Kwetu, shabaha ya mwaka 2030 ni yenye makuu, inafikika, na ya manufaa kwa Ulaya," aliongeza.
Shabaha hiyo kubwa inaungwa mkono na mataifa makubwa ya Ulaya ya Ufaransa na Ujerumani pamoja na kampuni kubwa, lakini itakubana na upinzani mkubwa kutoka mataifa ya Ulaya Mashariki yanayotegemea makaa ya mawe kwa mahitaji yao ya nishati.
Soma pia: Onyo dhidi ya kufumbia macho mabadiliko ya tabia nchi latolewa
Viongozi wa Umoja wa Ulaya walikubaliana mwaka uliyopita kuufanya uchumi wa kanda hiyo kuwa usiyokuwa na kaboni kufikia katikati mwa karne.
Von der Leyen ameongeza kwamba anataka asilimia 37 ya mfuko wa ufufuaji uchumi wa euro bilioni 750 uliyoidhinishwa na mataifa ya Umoja wa Ulaya majira ya msimu mwaka huu kutumika kwenye utekelezaji wa malengo ya kimazingira, na kwamba asilimia 30 ya fedha hizo inapaswa kukusanywa kupitia "dhamana za kijani", ambazo mapato yake yanakusudiwa kuwa na athari chanya kwenye mazingira.
Ahimiza ujasiri kwenye diplomasia
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amezikosoa serikali za mataifa ya umoja huo kwa kuwa na sera ya kigeni isiyo na ufanisi, na kupendekeza mfumo wa vikwazo kama wa Marekani dhidi ya wakiukaji wa haki za binadamu duniani.
Umoja huo ambao uliwahi kujivunia "nguvu yake laini" iliyosaidia kuyabadilisha mataifa jirani ya kikomunisti na kufungua masoko yake, hivi sasa unazidi kujikuta ukishindwa kukubaliana juu ya misimamo ya pamoja kushawishi diplomasia ya kimataifa, kuhusu masuala kuanzia Venezuela hadi Mali.
"Kwanini hata matamshi madogo kuhusu maadili ya Umoja wa Ulaya yanacheleweshwa, kupunguzwa makali au kushikiliwa mateka?" Alihoji von der Leyen katika hotuba yake. "Mataifa wanachama yakisema Ulaya inajikongoja, nawaambia 'kuweni majasiri na hatimaye msogee kwenye upigaji kura kwa wingi," alisema.
Upigaji kura wa mfumo huu utausaidia Umoja wa Ulaya kuchukuwa hatua juu ya masuala mengi zaidi bila kupitia mchakato mgumu zaidi wa kupata uungwaji mkono wa mataifa yote 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Soma pia:Maoni: Viktor Orban anaudhihaki Umoja wa Ulaya
Von der Leyen amesema Halmashauri kuu itakuja na pendekezo la kuzuwia mali na wale wanaozingatiwa kuhusika na ukiukaji wa haki za binadamu, unaofanana na sheria ya Magnitsky ya mwaka 2012 nchini Marekani.
Sergei Magnitsky alikuwa wakili wa Urusi aliekamatwa mwaka 2008 baada ya kudai kuwa maafisa wa Urusi walihusika katika kashfa kubwa ya udanganyifu wa kodi. Magnitsky alifariki katika gereza mjini Moscow mwaka 2009 baada ya kulalamikia kutendewa vibaya.
Soma pia: Mamlaka Misri zashutumiwa kuvunja haki za watumiaji mitandao
Mfumo mpya wa vikwazo utauwezesha Umoja wa ulaya kuweka vikwazi haraka zaidi dhidi ya watu makhsusi kokote duniani, kuzuwia mali zao zilizoko kwenye kanda hiyo, na kuwapiga marufuku kuingia kwenye kanda hiyo.
Uhamiaji, Uturuki na Brexit
Amzungumzia pia suala la uhamiaji, ambapo ameyatolea mwito mataifa ya Ulaya kushirikiana pamoja kuhusu suala hilo, baada ya moto kuunguza kambi ya wahamiaji nchini Ugiriki na kuwaacha maelf ya watu bila makaazi.
Kuhusu mzozo unaoendelea kati ya Uturuki kwa upande mmoja, na Ugiriki na Cyprus kwa upande mwingine, Von der Leyen amesema Uturuki ni mshirika muhimu na itaendelea kuwa hivyo, lakini akaongeza kuwa licha ya pande hizo mbili kuwa karibu kwenye ramani, umbali kati yao unaonekana kuzidi kuwa mkubwa.
Soma zaidi: Viongozi wa EuroMed7 wako tayari kwa vikwazo vya EU dhidi ya Uturuki
Rais huyo amelalamika kwmaba matumaini ya kufikiwa makubaliano na Uingereza baada ya nchi hiyo kujitoa katika Umoja wa Ulaya yanafifia na kuionya Uingereza kutoufanyia marekebisho kivyake mkataba wa kujiondoa. Ameeleza hofu kwamba kila siku inayopita, fursa za kufikia makubaliano kwa wakati zinazidi kufifia.
Chanzo: Mashirika