Ureno yatinga nusu fainali
22 Juni 2012Jamhuri ya Czech hawakuweza kufurukuta katika mchezo huo uliofanyika katika uwanja wa taifa mjini Warsaw na goli la kichwa la Cristiano Ronaldo katika dakika ya 79 ya mchezo huo ndio lililoipeleka timu hiyo ya taifa ya Ureno katika nusu fainali na kuweka miadi na mshindi wa pambano la siku ya Jumamosi kati ya Ufaransa na Uhispania.
Lakini Bilek amesema fadhaa ya kushindwa iliondoka kutokana na mafanikio ya kuunda kikosi ambacho ni mchanganyiko wa vijana chipukizi na wale wenye uzoefu, na pia kutokana na kumkosa mchezaji wa kiungo mchezeshaji Tomas Rosicky.
Mara tu baada ya mchezo huo tulijisikia kuvunjika moyo kwasababu tumepoteza mchezo, amesema Bilek.
Tulikuwa tunamatumaini ya kusonga mbele katika nusu fainali na hadi fainali na tulitaka hilo litokee. Tumecheza vizuri katika mashindano haya . Tumecheza dhidi ya wapinzani ambao ni hatari zaidi na walikuwa na nafasi nyingi. napenda kuwashukuru vijana wangu kwa mchezo wao, amesema Bilek.
Jamhuri ya Czech iliwahi kutamba
Jamhuri ya Czech ilikutana na Ureno mara sita katika mashindano makubwa , ikiwa ni pamoja na robo fainali katika mashindano ya euro 1996, wakati goli la ushindi la Karel Poborsky liliwapeleka katika nusu fainali na hatimaye fainali ambayo walipoteza dhidi ya Ujerumani.
Lakini wakiwa na timu ya sasa ambayo kwa kiasi kikubwa haina majina makubwa , mbali ya mlinda mlango wa Chelsea na ambaye ndie nahodha wa kikosi hicho Petr Cech, pamoja na Tomas Rosicky wa Arsenal pamoja na mshambuliaji anayekuja juu Vaclav Pilar, ni watu wachache sana waliokipa kikosi hicho cha Bilek nafasi kubwa ya kusonga mbele.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 47 ameelezea muda wake katika kukifunza kikosi hicho kuwa kama maporomoko na kukiri kuwa mafanikio yamevuka matarajio yake, wachezaji wake wakionyesha uwezo mkubwa wa kupambana baada ya kufungwa mabao 4-1 katika mchezo wa makundi dhidi ya Urusi iliyoonekana kuwa bora zaidi.
Ustadi ulikuwa ufunguo
Kocha wa Ureno Paulo Bento amesema kuwa ustadi ulikuwa ndio ufunguo wa ushindi wa kikosi chake katika mchezo huo.
Amekiri kuwa Ureno haikuanza vizuri katika ushambuliaji . Hatukuweza kuwa makini wakati tukiwa na mpira katika sehemu ya kwanza ya mchezo, amekiri.
Na baada ya hapo tuliweza kutulia na kudhibiti mchezo. Tulidhibiti mchezo katika aina ya pekee, tulicheza haraka na katika nusu ya pili tulionyesha uwezo mkubwa.
Nani atatamba
Jioni ya leo (22.06.2012) Ujerumani inaingia uwanjani kuumana na Ugiriki, katika mchezo wa pili wa robo fainali. Kocha wa Ugiriki Fernando Santos amesema kuwa ataunda masta plani ambayo itawavuruga Wajerumani katika robo fainali hii. Kocha wa Ujerumani Joachim Loew amesema nae kuwa anafahamu mbinu ya Ugiriki ya kulinda mno lango na kupiga mipira mirefu kwa mshambuliaji wao Samaras. Amesema kuwa wamejitayarisha kwa kila hali, na suala ni kusubiri na kuona kitakachotokea.
Mwandishi: Sekione Kitojo /Bruce Amani
Mhariri: Abdul-Rahman