Ureno yajiongezea taji la Ulaya
10 Juni 2019Ureno imeongeza taji jipya la ligi ya mataifa lililoanzishwa hivi karibuni katika taji lake la ubingwa wa Euro mwaka 2016 kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Uholanzi mjini Porto jana Jumapili.
Ulinzi pacha wa Virgil van Dijk na Matthijs de Ligt kwa kiasi kikubwa ulimtia mfukoni Cristiano Ronaldo , lakini mshambuliaji wa pembeni wa Valencia Gonzalo Guedes aliamua mchezo huo wakati shuti lake lilikuwa na nguvu kubwa na kumshinda mlinda mlango wa Uhloanzi Jasper Cillessen.
Ureno ilisherehekea kushinda ubingwa huo wa ligi ya mataifa ya bara la Ulaya kwa kuliwasilisha kombe hilo katika jengo la halmashauri ya jiji la Porto jioni ya jana Jumapili.
Maelfu ya mashabiki wa kandanda walimiminika katika eneo hilo na Cristiano ronaldo aliwashukuru mashabiki hao mjini Porto na Ureno kwa jumla.
"Kwa niaba ya timu ya taifa na wachezaji wenzangu wote, kwa niaba ya rais na makocha tungependa kuwapa nyie mashabiki asante sana kwasababu bila nyie isingewezekana kwa uungaji mkono mliotupatia katika mchezo wa kwanza dhidi ya Uswisi na pia leo."
Nae kocha wa Ureno Fernando Santos aliwashukuru pia mashabiki na wanachi wa Ureno kwa kuwapa nguvu kwa kuwaunga mkono. Na pia aliwashukuru wachezaji wake kwa furaha waliowapa mashabiki.
England imewasili katika nusu fainali za mashindano makubwa mawili lakini kocha Gareth Southgate amesema kushindwa kufikia fainali ya kombe la dunia na ligi ya mataifa imekiacha kikosi chake kikiwa hakijaridhika. Ushindi wa mikwaju ya penalti dhidi ya Uswisi jana Jumapili ulishuhudia England ikimaliza katika nafasi ya tatu katika mashindano hayo ya mwanzo ya ligi ya mataifa, nafasi moja bora kuliko kombe la dunia mwaka 2018 wakati waliposhindwa na Ubelgiji katika mchezo wa kuwania medali ya shaba.
Wakati huo huo kocha wa Uholanzi Ronald Koeman amesherehekea msimu mzuri na Uholanzi licha ya kipigo ilichokipata jana Jumapili katika fainali ya ligi ya mataifa ya UEFA.
Koeman amesema kipigo cha bao 1-0 dhidi ya wenyeji Ureno katika uwanja wa Estadio do Dragao hautaondoa kitu chochote katika kikosi chake kutokana na mafnikio yaliyopata timu yake katika kujijenga upya msimu huu.