1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upungufu wa malisho wazua mapigano ya wakulima na wafugaji

22 Machi 2016

Miongoni mwa mambo yanayochangia ongezeko la mapigano ya wakulima na wafugaji ni serikali ya Tanzania kuchukua ardhi kwa ajili ya hifadhi, rushwa, ufinyu wa miundombinu na uwekezaji katika kilimo.

https://p.dw.com/p/1IHSh
Wafugaji Sudan
Picha: Getty Images

Utafiti uliofanywa na Mtandao wa maliasili nchini Tanzania, TNRF, umebaini kuwa miongoni mwa mambo yanayoweza kuchangia kuongezeka kwa mapigano kati ya wakulima na wafugaji nchini humo, ni pamoja na serikali kuchukua ardhi kwa ajili ya hifadhi, kuongezeka kwa mahitaji ya uwekezaji kwenye sekta ya kilimo, rushwa na ufinyu wa miundombinu ya kuwezesha wafugaji kupata malisho ya kujitosheleza. Makundi hayo yamekuwa yakitupiana shutuma za mara kwa mara ambazo mara nyingine zimeibua mapigano kati yao.

Utafiti huo umefanywa mwaka 2014 nchini Tanzania, na kubaini kuwa wafugaji ambao wengi wao ni matajiri huwatuhumu wakulima, na kuwapa rushwa viongozi wa vijiji ili wawaruhusu kuingiza mifugo yao kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kilimo.

Wale wanaouana sio waliosababisha matatizo, na huu ndio ukweli ambao hata wao hawaujui, alisema Godfrey Massay, mratibu wa masuala ya uwekezaji kwenye mtandao huo. Akaongeza kuwa, "Nikiwaona wakulima na wafugaji wakipigana, kwa kweli nashindwa kupata msingi wa sababu za mapigano hayo kutokea."

Rushwa yachochea mapigano

Ikolongo ni miongoni mwa vijiji vilivyoko Mkoani Iringa, katika nyanda za Juu za Kusini mwa Tanzania, ambako kunakabiliwa na mapigano ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji, wakigombania maji. Ukame wa muda mrefu unawasukuma wafugaji , ambao mara nyingi hukaa milimani, kushuka chini ili kutafuta maji kwenye mito midogo, ambako ndiko kwenye wakulima wengi.

Uhaba wa maji ni changamoto kwa wakulima na wafugaji Südafrika Dürre Wasserverteilung - 11 January 2016 epa05096910 Residents queue for water at a distribition point in the rural farming town of Senekal, South Africa, 11 January 2016. The water is being trucked to the town by local government sources. The town last had rain on 15 December 2015 and has had a severe water shortage for the past 3 months with residents having to queue for water at water hand out points. Large parts of this district and widespread areas of South Africa are experiencing the worst drought in 30 years as well as the highest temperatures in decades. EPA/KIM LUDBROOK EPA/KIM LUDBROOK (c) picture-alliances/dpa//K. Ludbrock
Uhaba wa maji ni changamoto kwa wakulima na wafugajiPicha: picture-alliances/dpa//K. Ludbrock

Mapigano ambayo mara nyingine huzuka kati ya makundi hayo mawili, yanaweza yakasababisha vifo. Mwezi wa pili, mtu mmoja aliuwawa na wengine wakijeruhiwa, ambao miongoni mwao ni polisi wawili, kwenye mapigano yaliyotokea kijiji cha Dihia, wilaya ya Morogoro Vijijini.

Hata hivyo, mapigano haya kwa sasa ni historia. Kwenye kijiji cha Pawaga, wakulima na wafugaji wamekubaliana kumaliza tofauti zao zilizodumu kwa muda mrefu kwa njia rahisi tu ya mazungumzo. Wamekubaliana kwa pamoja kusuluhisha migogoro yao kwa mazungumzo, chini ya Mtandao huo wa maliasili, TNRF, unaojaribu kujenga maelewano kati ya makundi hayo kuhusiana na mahitaji yao, na kuwahamasisha kutafuta namna mbadala ya kupata suluhu ya migogoro.

Tayari makundi hayo mawili yameafikiana maeneo ambayo wafugaji watapeleka mifugo yao kunywa maji bila ya kuathiri mahitaji ya maji ya wakulima. Makundi hayo hihi sasa hukutana mara mbili kila mwezi bila ya kuwa na hofu, na kujadili suala lolote linalojitokeza.

Mazungumzo ya kuleta suluhu yahitajika

Kulingana na TNRF, pamoja na maamuzi ya kugawana, makundi hayo mseto tayari yamebaini na kuwaibua watoa rushwa waliokuwa wananchochea mapigano kati yao. Aidha, Wanakijiji hao wamewaweka hadharani viongozi wa vijiji waliokuwa wakipokea rushwa kutoka kwa wafugaji , na wakati huohuo wakila njama na wakulima na polisi ili kuwakamata walioingia kwenye ardhi ya mashamba. "Wakulima na wafugaji wanahitaji kuelewa kuwa kuna watu wanaonufaika na mizozo miongoni mwao, ambao pia hawataki kuona inapatiwa ufumbuzi," alisema Massay.

Serikali imetakiwa kuweka mpango maalum wa matumizi ya ardhi
Serikali imetakiwa kuweka mpango maalum wa matumizi ya ardhiPicha: picture alliance/africamediaonline

Henry Mahoo, Profesa wa masuala ya kilimo kwenye chuo kikuu cha kilimo cha Sokoine, amesema mashirikiano kama haya ni muhimu katika kutafuta suluhisho la kudumu la mapigano juu ya maji na ardhi. Migogoro kati ya wakulima na wafugaji inaweza kutatuliwa kwa kuwepo na mpango maalumu wa matumizi ya ardhi, utakaoweka wazi maeneo yatakayotumiwa na makundi hayo. Tanzania ina zaidi ya kilomita za mraba 611,200 za malisho ya mifugo, na asilimia 70 ya ardhi hiyo inatumiwa na wafugaji, wakati iliyosalia iko kwenye hifadhi ya serikali.

Mwandishi: Lilian Mtono.

Mhariri: Saumu Yusuf.