Upinzani Zimbabwe wataka serikali ya mpito
24 Oktoba 2018Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Zimbabwe Nelson Chamisa ametoa wito jana wa kuundwa serikali ya mpito kutatua hali mbaya ya kiuchumi na mzozo wa kisiasa unaoikumba nchi hiyo. Upungufu wa fedha za kigeni katika wiki za hivi karibuni umezusha mzozo mkubwa wa kiuchumi ambapo upatikanaji wa mafuta , chakula na madawa unapungua. Hatua ya kwanza ni kwa nchi hii kuingia katika njia ya mjadala wa kisiasa, amesema chamisa mwenye umri wa miaka 40, kiongozi wa chama cha Movement for Democratic Change MDC, ambaye amedai kwamba ameshinda uchaguzi wa rais wa hapo Julai 30. Chamisa ambaye alishindwa na rais wa sasa Emmerson Mnangagwa , amesema amekutana na viongozi wa kidini ambao wanataka mjadala wa kisiasa kati ya upinzani na rais.