Upinzani Zimbabwe wapinga ushindi wa Mnangagwa kortini
11 Agosti 2018Chama cha upinzani nchini Zimbabwe cha Movement for Democratic, MDC kimeenda mahakamani kwa lengo la kukata rufaa, ikiwa ni jaribio la kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais.
MDC kinadai kwamba kulifanyika udanganyifu kwenye matokeo hayo ili kuhakikisha kwamba yanampa ushindi rais Emmerson Mnangagwa.
Kiongozi wa MDC Nelson Chamisa amesema timu ya mawakili imefaulu kuwasilisha nyaraka za kesi hiyo katika mahakama ya kikatiba. Anataka mahakama imtangaze mshindi wa uchaguzi wa rais au iitishe ushaguzi mpya.
Hatua hiyo inakuja baada ya Chamisa, mwenye umri wa miaka 40 kupoteza kwa kura chache uchaguzi wa Julai 30 dhidi ya rais wa sasa Emmerson Mnangagwa.
Matokeo ya tume ya uchaguzi yalionyesha kuwa Mnangagwa alipata asilimia 50.8 ya kura akifuatwa na Chamisa akiwa na asilimia 44.3. Lakini Chamisa anadai alipata asilimia 56 ya kura.