1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani watangaza kuunda vuguvugu la kuilinda Tunisia

Mjahida24 Desemba 2014

Mgombea wa Urais aliyeshindwa katika dura ya pili ya uchaguzi wa Tunisia Moncef Marzouki ametangaza kuunda vuguvugu la kuizuwiya nchi hiyo kurejea katika utawala wa kidikteta.

https://p.dw.com/p/1E9lE
Rais wa Zamani wa Tunisia Moncef Marzouki
Rais wa Zamani wa Tunisia Moncef MarzoukiPicha: F. Belaid/AFP/Getty Images

Moncef Marzouki aliwambia maelfu ya wafusi wake kwamba ataunda vuguvugu la wa tu katika miji yote nchini humo ili kulinda mustakabal wa Tunisia huku akiwataka wafuasi wake kujipanga kwa njia ya amani na kidemokrasia.

"Nawaomba nyote mujumuike katika vuguvugu hili kubwa la kisiasa kazi yake ni kuongoza mustakbali wa Watunisia. Nitakuwa nanyi wakati wote na mahali popote," Moncef Marzouki.

Ameongeza kuwa vuguvugu hilo litaizuwiya nchi hiyo kurejea tena katika hatari ya kutawaliwa na watu walio na siasa kali kwa kuwa wanasiasa wengi walioingia madarakani ni maafisa waliohudumu katika serikali zilizopita.

Aidha Rais mteule, Beji Caid Essebsi aliye na miaka 88, alichaguliwa kama rais mpya wa Tunisia siku ya Jumapili baada ya uchaguzi wa marudio uliomaliza kipindi cha mpito nchini humo tangu kuanza kwa viguvugu la maandamano la kutaka mageuzi mwaka wa 2011.

Rasi wa Tunisia Beji Caid Essebsi na Moncef Marzouki
Rasi wa Tunisia Beji Caid Essebsi na Moncef Marzouki

Kuchaguliwa kwake kumepongezwa na viongozi wengi wa Magharibi akiwemo Rais Barrack Obama wa Marekani na Francois Hollande wa Ufaransa, huku Umoja wa Ulaya ukitangaza hapo jana kwamba Tunisia kwa mara ya kwanza imeandaa uchaguzi ulio huru na wazi.

Hofu ya kurejea utawala wa Kidikteta yatanda Tunisia

Essebsi alihudumu katika utawala wa marais waliopita nchini Tunisia na chama chake kimejaa maafisa wa utawala wa zamani hali inayoleta hofu ya kurejea tena kwa utawala wa kidikteta.

Hata hivyo, Essebsi amesema kamwe Tunisia haiwezi kurejea katika utawala wa kizamani au katika mambo ambayo ni historia.

Kwa sasa, miongoni mwa changamoto kubwa zinazomkabili rais huyo mpya ni kudhibiti makundi ya kigaidi na kuimarisha maendeleo ya nchi, kama anavyosema Khaleed mmoja ya wakaazi katika mji mkuu Tunis.

Raia wa Tunisia wakipeperusha bendera ya nchi hiyo
Raia wa Tunisia wakipeperusha bendera ya nchi hiyoPicha: Getty Images/AFP/B. Taieb

"Changamoto inamkabili rais wa sasa ni kwanza kukabiliana na ugaidi na la pili ana upinzani mkali na lazima aingalie namna ya kuleta umoja ndani ya serikali na pia uchumi ni jambo gumu linalomkabili rais huyu wa sasa,"alisema Khaleed.

Rais Essebsi anatarajiwa kuunda serikali baada ya chama chake cha Nidaa kushinda pia katika uchaguzi wa bunge uliofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef