1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani wasitisha maandamano Venezuela

2 Novemba 2016

Wapinzani nchini Venezuela wamesitisha mashtaka bungeni pamoja na maandamano yaliyokuwa yamepangwa dhidi ya Rais wa nchi hiyo Nicolas Maduro, ili kupisha mazungumzo ya wiki ijayo.

https://p.dw.com/p/2S359
Venezuela Proteste in Caracas
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Cubillos

Spika wa Bunge la kitaifa ambalo linatawaliwa na upinzani Ramos Allup, alisema kuwa uamuzi huo wa kusitisha kesi dhidi ya rais Maduro ambaye anashutumiwa kukiuka majukumu yake ya kikatiba, haimaanishi kuwa wamesalimu amri, na badala yake imeonyesha ari ya upinzani katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo kwa njia ya mazungumzo na Serikali, ambayo yamepangwa kufanyika Novemba 11 alisema spika huyo, na kuongeza kuwa maandamano kuelekea katika ikulu ya rais yaliyopangwa kufanyika siku ya Alhamis pia yameahirishwa

Wachambuzi wanaiita kesi hiyo dhidi ya Maduro kuwa ilikuwa ni ishara ya ubora tu, kwa sababu katiba ya nchi hiyo hairuhusu kuchukuliwa kwa hatua hiyo dhidi ya rais. Maduro mwenyewe amepuuzia juhudi hizo na kusema ni juhudi batili za kutaka kuipindua serikali yake, na kuapa kuwaweka jela wahusika wote.

"Nakaribisha ukweli kuwa upinzani umeamua kuchukua maamuzi ya busara, nakaribisha hilo" alisema rais Madulo wakati akizungumza katika kipindi chake cha wiki cha televisheni na kuongeza kuwa, "nilishikana mkono na Chuo Torrealba, sikumpenda kabisa na sasa ninampenda ni mtu mzuri" akimaanisha kiongozi wa muungano wa vyama vya upinzani wa Democratic Unity Roundtable, MUD.

Venezuela Nicolas Maduro
Rais wa Venezuela Nicolas MaduroPicha: picture alliance/abaca/C. Becerra

Wapinzani wasema majadiliano ni njia sahihi

Kupungua kwa shinikizo dhidi ya Maduro inaonyesha kuwa wapinzani wanaona kuwa majadiliano ni njia sahihi, badala ya kutumia nguvu kujaribu uwezo wao kwa kuuleta umma upande wao kwa maandamano.

Utafiti unaonyesha kuwa Maduro hivi sasa hakubaliki na Wavenezuela kwa zaidi ya asilimia 75. Wengi wanalaumu hali mbaya inayowakabili kwa rais huyo ambaye muhula wake unamalizika mwishoni mwa mwaka 2019, na uamuzi wake wa kudumisha sera za kisoshalisti ambazo zilitangazwa na mtangulizi wake Hugo Shavez ambazo zimekuwa na matokeo katika kushuka kwa bei ya mafuta ambayo ni rasilimali ya kutegemewa nchini humo.

Lakini Wavenezuela wanaelekeza zaidi muda wao siku hizi katika kupanga foreni za mahitaji muhimu muhimu  badala ya kujitosha mitaani kudai mabadiliko wakati ambao wanasumbuliwa na upungufu mkubwa wa chakula, huduma ya nishati ya umeme na huduma bora za afya katikati ya mfumuko mkubwa wa bei.

Marekani ambayo imekuwa na mahusiano ya kusuasua na Maduro pamoja na mtangulizi wake Hugo Shavez imejitosa pia kuunga mkono mazungumzo hayo pamoja na kuwa, baadhi ya wachambuzi wanaonya kuwa huenda serikali imekubali mazungumzo ili kupoteza muda.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga