Upinzani washinda Poland
22 Oktoba 2007Kiongozi wa upinzani Donald Tusk alisubiri kwa muda mrefu hadi kushangiliwa kama mshindi wa uchaguzi jana usiku. Ameshawahi kushindwa katika uchaguzi wa rais, hata ndani ya chama chake cha “jukwaa la raia”, PO, ana wapinzani. Sasa lakini chama hiki cha kiliberali kitachukua zaidi ya asilimia 40 ya viti vya bunge. Bw. Tusk bado hajatangaza ni chama gani anachotaka kutawala nacho.
Alipozungumza mbele ya wafuasi wake jana usiku, Tusk alisema: “Ninawashukuru wote ambao walisaidia kuuonyesha Umoja wa Ulaya kwamba sisi Wapoland tunaweza kuchukua jukumu wakati inapohitajika. Ushahidi wake ni kwamba idadi ya watu waliopiga kura ni haijawahi kuwa kubwa kama leo tangu kumaliza kwa enzi ya ukomunisti.”
Chama cha PO kina mradi wa kiliberali wa kiuchumi. Kinaunga mkono ubinafsishaji wa mashirika na kinataka sarafu ya EURO itumike haraka nchini Poland. Katika sera za nje, serikali chini ya Donald Tusk inatarajiwa kutumia maneno mazuri zaidi katika kuzungumza na washirika wake wa Umoja wa Ulaya, lakini wakati huo huo itatetea maslahi ya Poland katika Umoja wa Ulaya.
Katika kampeni yake ya uchaguzi, Donald Tusk pia alisema anataka jeshi la Poland lililotumwa Iraq lirudishwe nyumbani haraka licha ya Poland kuwa mshirika wa karibu wa Marekani.
Waziri mkuu Jaroslaw Kaczynski alikubali kushindwa. Bila ya kuonyesha hisia zake alimpongeza Donald Tusk na aliweka wazi kwamba: “Tutaunda upinzani mkali na tutachunguza ikiwa ahadi zitatekelezwa. Kwani kulitolewa ahadi za ajabu ajabu hapa kuhusu uchumi na bajeti ya Poland. Sisi tutaangalia kwa makini yale yatakayofikiwa.”
Licha ya Jaroslaw Kaczynski kugeuka upande wa upinzani, ndugu yake pacha Lech anabakia kuwa rais. Muda wake madarakani utaisha mwaka 2010 na serikali mpya italazimishwa kupatana naye kwa vile rais ana haki ya kupiga kura ya turufu. +
Nchi za Umoja wa Ulaya zimepokea vizuri ushindi wa Donald Tusk. Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alisema ana matumaini kwamba uhusiano kati ya Ujerumani na Poland utaboreka na kwamba nchi zote mbili zinaungana katika Umoja wa Ulaya.
Hans-Gert Pöttering ambaye ni spika wa bunge la Ulaya, katika mahojiano na Redio Deutsche Welle alimsifu Donald Tusk na alisema: “Yeye anauunga mkono muungano wa Ulaya na ninaamini huu ni msingi mzuri kwa Umoja wa Ulaya kujiendeleza zaidi. Kitu kinachofurahisha sana ni kuwa idadi ya vijana waliopiga kura ni kubwa sana. Hivyo walionyesha kuwa kizazi kipya kinataka Umoja wa Ulaya uimarishwe. Hiyo ni ishara nzuri sana.”
Hatua inayotarajiwa kufuata sasa ni kwa rais Lech Kaczynksi kumuagiza Donald Tusk aunde serikali mpya ya Poland.