Upinzani wapata nguvu Venezuela
25 Novemba 2008Tangu kupita miaka mingi,Upinzani nchini Venezuela sasa una nafasi nzuri kabisa ya kutoa changamoto kali kwa Rais Hugo Chavez kufuatia ushindi wao katika chaguzi za mikoa mwishoni mwa wiki.Hatahivyo, utahitaji kujenga uongozi imara zaidi kitaifa na jukwaa la sera zake.
Ushindi mkubwa wa Upinzani katika miji, una maana kwamba viongozi wake waweza kutumia kuvunjika moyo na kufadhahika kwa mitaa ya majengo-poromoka kwa kubainisha waweza kupambana na matatizo yanayowakumba wananchi katika maisha ya kila siku.
Mafanikio katika kukabiliana na maswali kama hayo ,kungewapa viongozi wa Upinzani nchini Venezuela, nafasi bora ya kumyumbisha rais Hugo Chavez na kuondoa matumaini yake ya kuendeleza zaidi utawala wake kupindukia mwaka 2013 pale kipindi chake cha sasa cha utawala kitakapomalizika.
Mkusanyika wa vikundi mbali mbali kama vile vya wanafunzi wakereketwa,wamangimeza na wanasiasa wa zamani wataweza tu kuwa kitisho kwa rais Chavez ikiwa tu watajipatia mwanasiasa atakaekuwa nyuma yao.
Au kuwa na mradi wa kisiasa utakaoshindana na na mapinduzi yake ya kijamaa.
Rais Chavez ,msoshalist anaepinga sera za Marekani hachelei kuwadhofisha viongozi wa mikoa kwa kuwakatia fedha na kutumia njia za kisheria kuwaweka nje ya madaraka na kuwateua maafisa wa mikoa wenye madaraka makubwa zaidi katika nchi hii mwanachama wa Umoja wa OPEC.
Wafuasi wa rais Chavez walishinda mikoa 17 kati ya yote 22 katika uchaguzi wa mwishoni mwa wiki.Na hii imeonesha kuendelea kwa umaarufu wake . Viongozi wa vyama vya Upinzani walishinda katika baadhi ya mikoa kwa kuiteka mikoa 5 na miji mikuu 3 ya dola hili lanachama wa Umoja wa nchizinazosafirisha mafuta ulimwenguni (OPEC).Hiyo ni mikoa ambayo kwa jumla, ina nusu ya wapigakura wote wa Venezuela.
"Kuanzia sasa yatupasa kusonga mbele na kugeuka kutoka kuwa wapinzani wa Chavez na kuwa jukwaa linalolilia mustakbala mwema kwa Venezuela."-alisema Leopoldo Lopez,kijana-maarufu kutoka Upinzani.Isitoshe, viongozi wapya wa Upinzani waache kutotiwa kitunga cha macho na siasa za kitaifa na kusahau shida za siku kwa siku za wananchi mikoani.
Uchaguzi wa jumapili uliendeleza nguvu za upinzani kwenye uchaguzi wa nchi hii kufuatia ushindi wao wa Desemba mwaka jana walipoyatia munda mageuzi ya rais Chavez katika kura ya maoni-mageuzi ambayo yangepanua zaidi madaraka yake.
Ushindi wa upinzani mwishoni mwa wiki, umefufua upinzani ambao vyama vyao vya desturi vilipigwa kumbo pale rais Chavez aliponyakua madaraka 1999 na kupata mapigo kama vile kosa la njama ya kumpindua Chavez ya 2002,mgomo wa miezi 2 wa viwanda vya petroli na kususiwa kwa uchaguzi 2004 na tena 2005.
Kuanguka sasa kwa bei za mafuta ya petroli kunatishia kuporomoa miradi ya Chavez anayokusudia kuigharimia kutokana na pato la mafuta na hivyo kukuza umaarufu wake huku akihimiza mageuzi yatakayomuwezesha kugombea tena uchaguzi.
Upinzani lakini umegawanyika huku hakuna chama kimoja kikishinda zaidi ya mkoa mmoja katika uchaguzi wa jumapili iliopita na havina uongozi bora kumshinda rais Chavez unawafikia hata wakaazi wa mitaa ya mbali ya madongo-poromoka.
Rais Chavez ana uwezo wa kuwashinikiza magavana wa mikoa wanaoitegemea mno serikali kuu kwa mgawao wake kutoka pato la mafuta.Nae amechukua hatua kuudhofisha upinzani na mnamo miezi ya karibuni ,ameondoa dhamana za mahospitali na kikosi cha polisi cha mji mkuu Caracas kutoka dhamana za diwani wa mji .Amepitisha kanuni zinazomuwezesha kuwateua maafisa wanaoweza kuendesha shughuli za wapinzani.
"Venezuela ina mfumo wa utawala wa serikali kuu ambamo magavana wa mikoa na mameya hawana usemi mkubwa."-adai Patrick Esteruelas wa Taasisi ya Eurasia mjini New York.