Upinzani wamshutumu Tshisekedi kuanzisha kampeni ya mapema
4 Januari 2022Upinzani unashutumu matumizi ya rasilimali za nchi na fedha za walipa kodi, kwa kufanya mapema kampeni ya uchaguzi, ilhali akiwa mkuu wa nchi, Rais Tshisekedi alipaswa kuwa mfano wa kuheshimu sheria, kama anavyoeleza Prince Epenge, mmoja wa wasemaji wa muungano wa upinzani wa Lamuka.
"Akifahamu kuwa hawezi kupewa na muhula wa pili, anajaribu kuficha kushindwa kwake akitumia fedha za serikali kwa shughuli zake binafsi. Kipindi cha kampeni bado hakijaanza. Anaweza kuzurura Jamhuri anavyotaka kwa sababu ameenda kuhisi kushindwa kwake", asema Epenge.
Soma pia:Congo itakuwa mwanachama rasmi wa EAC
''Anafanya kampeni akitumia mali ya umma''
Kwa upande wa chama cha MDVC, chake Justin Mudekereza, kilichokuwa kikimkosoa Tshisekedi kuhusu ziara nyingi alizozipa kipaumbele katika nchi za kigeni na bila ya matokeo chanya, sasa kimefurahishwa na ziara ya rais huko Kasai, lakini pia inalaani kuanza mapema kampeni ya uchaguzi, wakati bado sheria haijaruhusu.
Na hivyo, chama hicho kinatishia kumshtaki Rais Félix Tshisekedi, kama anavyohakikisha Augustin Bisimwa, Katibu Mkuu wa MDVC.
"Tutalifikisha jambo hili mahakamani kwa sababu hawezi kuanza kampeni kabla ya wakati. Tatizo kubwa ni kwamba anafanya kampeni yake akitumia mali ya umma.''alisema Bisimwa.
''Tumeona wanatumia magari pamoja na feza za Serikali, yaani kila kitu cha serikali. Tumetambua kwamba katika hotuba zake anaomba tu, muhula wa pili", aliendelea kusema.
Tukumbushe kwamba Kasai ndilo eneo anamotoka Félix Tshisekedi. Ziara yake hii ambayo bado inaendelea, imekuja miaka mitatu baada ya kuchaguliwa kwake kama rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.