Upinzani walalamika Angola
8 Septemba 2008Chama hicho tawala nchini Angola kimepata asilimia 81.8 ya kura zilizohesabiwa mpaka hivi sasa ambazo ni asilimia 70 ya kura zote.
Chama kikuu cha upinzani cha UNITA kimesema kuwa watu walilazimishwa kukipigia kura chama tawala katika uchaguzi huo uliyofanyika Ijumaa iliyopita, ambapo kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotolewa na tume ya uchaguzi nchini Angola ni kwamba kimepata ushindi mkubwa zaidi.
Ushindi huo ni pamoja na viti katika jimbo la Huambo ambalo lilikuwa ngome kuu ya UNITA , na hivyo kuwa na wingi wa theluthi mbili katika bunge la nchi hiyo lenye viti 220.
Lakini Rais wa UNITA Isaias Samakuva amelalamika kuwa uchaguzi huo ulikuwa na hila kubwa dhidi yao.
´´Katika vituo vingi vya kupigia kura uchaguzi ulifanyika bila ya kuwepo kwa uhakiki wa wapiga kura, hakukuwepo na majina ya wapiga kura katika karatasi au kwenye mfumo wa digital.Huu ni ukiukwaji wa sheria za uchaguzi kwamba ni lazima mpiga kura atambuliwe na kuwepo na utaratibu wa kumzuia kutopiga kura zaidi ya mara moja. hayo ndiyo masharti ya tume ya uchaguzi, lakini hayakufuatwa.´´
Uchaguzi huo uliyofanyika Ijumaa ulilazimika kuendelea hadi Jumamosi kutokana na ucheleweshwaji na mparaganyiko katika baadhi ya vituo kwenye mji mkuu wa nchi hiyo Luanda ambao una asilimia 21 ya wapiga kura wote millioni 8.3 nchini Angola.
Jumuiya ya kimataifa imekuwa ikifuatilia kwa karibu uchaguzi huo, ambapo waangalizi kutoka Jumuiya ya nchi zinazozungumza lugha ya Kireno CPLP imesema kuwa hakuna sababu ya kutilia shaka matokeo ya uchaguzi huo kwani kila kitu kilikwenda vizuri.
Leonardo Simao ambaye ni Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Msumbiji ni kiongozi wa ujumbe huo.
´´Naamini kuwa kila raia alipata nafasi ya kupiga kura kwa uhuru.Kampeni za uchaguzi zilifanyika kwa uvumilivu na kustahamiliana miongoni mwa vyama vilivyoshiriki.´´
Waangalizi kutoka Afrika Kusini na wale wa nchi za SADC pia walisema kuwa uchaguzi huo ulifanyika kwa amani, utulivu na haki.
Hata hivyo waangalizi kutoka bunge la Umoja wa Ulaya wamekosoa kasoro kadhaa katika uchaguzi huo, ikiwa ni pamoja na kutokuwepo kwa uhuru wa kujieleza.
Anna Gomes ni mbunge wa bunge hilo la Ulaya ambaye ni miongoni mwa waangalizi kutoka Ulaya aliyekuwa katika jimbo la Cabinda
´´Nimebaini ya kwamba hapa Luanda pamoja Cabinda wananchi pamoja na vyombo vya habari havikuwa huru.Hili ni lazima libadilishwe.´´
Hata hivyo ripoti rasmi ya Umoja wa Ulaya juu ya uchaguzi huo inatarajiwa kutolewa baadaye hii leo.