Upinzani wadhibiti kampuni ya mafuta Venezuela
14 Februari 2019Wakati Marekani ikiishinikiza serikali ya Venezuela kuruhusu misaada ya kiutu kuingia nchini humo, upinzani unaolidhibiti bunge la nchi hiyo umeteuwa bodi ya mpito ya kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali, ikiwa ni jitihada za kuingozi wa bunge hilo Juan Guaido kuidhibiti sekta ya uchimbaji wa mafuta, ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi hiyo. Sudi Mnette anaarifu juu ya hayo yanayojitokeza nchini Venezuela.
Guaido, ambae Januari 23 alijitangaza kuwa rais wa mpito wa Venezuela, huku akiungwa mkono na Marekani na idadi kubwa ya mataifa Amerika ya Kusini, amesema bodi hiyo mpya itafuatilia mwenendo wa kampuni ya mafuta ya Kimarekani ya PDVSA, yenye kiwanda chake cha kusafisha mafuta, huko Houston kiitwacho Citgo.
Kunyong'onyesha nguvu za kidikteta
Guaido ambae anaongoza jitihada kabambe ya kumondoa madarakani rais msoshalisti Nicolas Maduro, amenukuliwa katika ukurasa wake wa twitter akisema "Uokozi wa kiwanda chetu cha mafuta imeanza. CITGO ni kwa aajili ya Venezuela." Mwakilishi wa kiongozi huyo akiwa mjini Washington, Carlos Vacchio, amesema operesheni za kampuni itaendelea kuongozwa na waajiriwa walewale waliopo.
Aidha ameongeza lengo la hatua ya kubadilisha uongozi ni kuidhibiti kampuni hiyo isendelee kutumiwa na nguvu za kidikteta. Hata hivyo maafisa wa kampuni hiyo pamoja na wengine wa wizara ya mawasiliano nchini Venezuela hawakuweza kupatikana mara moja kwa lengo la kulitolea ufafanuzi suala hilo. Awali rais Maduro aliituhumu Marekani na upande wa upinzani wa Venezuela kujaribu kupanga njama za mapinduzi dhidi yake.
Trump amuonya Maduro
Katika hatua nyingine Rais Donald Trump wa Marekani ameitaka Venezuela kuruhusu msaada wa chakula kuingia katika taifa hilo, ikionya kwamba serikali yake ina namna lakini ikikwepa kueleza moja kwa moja kuzungumzia uwezekano wa matumizi ya kijeshi. Akizungumza katika ikulu ya Marekani-White House- Rais Trump amesikika alisema "Tunajaribu kufikisha chakula kwa watu wanaokabiliwa na njaa." Na kuongeza kuwa kuzuia misaada hiyo ni jambo linaloonekana kama uhalifu dhidi ya ubinaadamu.
Akizungumza baada ya mkutano wa Rais Trump na kiongozi wa Colombia Ivna Duque, Rais Maduro alikuwa na haya ya amesema "Leo hii rais wa Marekani Donald Trump amekutana na Ivan Duque wa Colombia ikiwa kama siku ya chukizo. Kama mtu atayatazama macho yake, muonekano, maneno, na taarifa yake, muonekano wa chuki dhidi ya Venezuela, akizungumza mambo ya hovyo dhidi ya Venezuela."
Katika mkutano wake huo Rais Trump amesema Maduro ana sababu kadhaa zinazoweza kumfanya ajiuzulu kama rais wa Venezuela. Lakini pale alipoulizwa kama Marekani ina lengo la kupeleka wanajeshi 5,000 nchini Colombia alijibu kuwa "Utakuja kuona." Kwa hivi sasa serikali ya Maduro imezuia tani 100 ya shehena ya misaada ya kiutu kutoka Colombia, ikitoa sababu kuwa ni hatua ya awali ya uingiliwaji wa kijeshi.
Mwandishi: Sudi Mnette DPA/APE
Mhariri: Grace Patricia Kabogo