Upinzani wadai ushindi katika uchaguzi wa Zimbabwe
30 Machi 2008Chama cha upinzani nchini Zimbabwe cha Movement for Democratic Change, MDC, leo kinadai kimeshinda uchaguzi uliofanyika jana nchini humo. Katika matokeo ya awali msemaji wa chama hicho, Tendai Biti, amesema kiongozi wa chama cha MDC, Morgan Tsvangirai huenda akashinda asilimia 66 ya kura katika mji mkuu Harare, ambao ni ngome ya upinzani.
Amesema kiongozi huyo amepata idadi kubwa ya kura katika ngome za rais Robert Mugabe kwa kuongoza katika mkoa wa kusini wa Masvingo na mkoa wa kati wa Mashonaland, kaskazini mwa Harare, ambako chama cha MDC hakijashinda kiti cha ubunge tangu mwaka wa 2000.
Tsvangirai pia ameshinda katika jimbo la Mashonaland magharibi, nyumbani kwa rais Mugabe, ambako chama cha MDC kimeshinda kiti cha ubunge. Tsvangirai pia anaongoza mbele ya Simba Makoni katika mji wa Bulawayo. Tsvangirai amesema hata ikiwa chama chake kitashinda, uchaguzi huo hauwezi kuelezwa kuwa ulifanyika kwa njia huru na ya haki.
Mizengwe
Upinzani nchini Zimbabwe umemshutumu rais Robert Mugabe kwa kufanya mizengwe katika uchaguzi wa jana. Waangalizi wa kiafrika pia wamesema wameshuhudia visa vya udanganyifu katika uchaguzi huo. Rais Mugabe, ambaye amekuwa madarakani tangu Zimbabwe ilipopata uhuru kutoka kwa Uingereza mnamo mwaka wa 1980, amekabiliwa na upinzani mkali katika uchaguzi wa jana kutoka kwa kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai na waziri wa fedha wa zamani wa chama cha ZANU-PF, bwana Simba Makoni.
Wakati vituo vya kupigia kura vilipofungwa, kiongozi wa chama MDC, bwana Tsvangirai, amesema wapigaji kura na maafisa wao walizuiliwa kuingia katika vituo hivyo na wino unaoweza kufutika ulitumiwa ili kuwezesha udanganyifu kwa upande wa wafuasi wa serikali.
Waangalizi wa bunge la Afrika wamesema katika barua yao walioiandikia tume ya uchaguzi ya Zimbabwe kwamba wamegundua watu zaidi ya 8,000 walioandikishwa katika ardhi ambayo haikaliwi na watu katika jimbo moja la mji mkuu Harare.
Rais Mugabe lakini amekanusha madai yote ya kuwepo udanganyifu. Matokoe ya awali yanatarajiwa kuanza kutangazwa hapo kesho.