1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chadema walalamika wagombea wake kuenguliwa kiholela

20 Novemba 2024

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Demokrasia na Maendelea kimelalamika kwamba wagombea wake wengi "wameenguliwa kwa njia zisizo za haki" kuwania katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakafanyika wiki ijayo.

https://p.dw.com/p/4nCGC
Tanzania | Freeman Mbowe
Kiongozi Mkuu wa CHADEMA Freeman MbowePicha: Ericky Boniphace/DW

Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Demokrasia na Maendelea, CHADEMA, kimelalamika kwamba wagombea wake wengi "wameenguliwa kwa njia zisizo za haki" kuwania katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakafanyika wiki ijayo. 

Taifa hilo la Afrika Mashariki litafanya uchaguzi wa viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji tarehe 27 Novemba unaotazamiwa kuwa kipimo cha hali ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, Oktoba mwaka unaokuja.

Soma pia: Mbowe: Mifarakano ya CHADEMA ni jambo la kawaida 

Kiongozi Mkuu wa CHADEMA, Freeman Mbowe amesema chama chake kilipanga kusimamisha asilimia 65 ya wagombea kuwania nafasi 80,430 zitakazopigiwa kura lakini hivi sasa ni asilimia 33 tu ya wagombea wake ndiyo wameidhinishwa.

Amesema wengi wamezuiwa kuwa wagombea kwa sababu alizosema kuwa "hitilafu ndogo ndogo" kama kukosa mihuri, kukosea majina na ukamilishaji wa fomu. Mbowe amelaumu kuwa wagombea wao wengi wameenguliwa kwa njia zinazokiuka kanuni za uchaguzi na dhamira ya makusudi ya wasimamizi wa uchaguzi.

Uchaguzi huo wa wiki ijayo utakuwa wa kwanza chini ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyeingia madarakani kufuatia kifo cha mtangulizi wake John Magufuli mwaka 2021.